Habari

Ogamba akemea wanasiasa kwa kuingilia uteuzi wa wanafunzi

Na TITUS OMINDE Na BARNABAS BII  January 10th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Elimu, Bw Julius Migos Ogamba, amewataka wanasiasa kujitenga na masuala ya elimu, akiahidi kulinda uadilifu wa zoezi la kuteua wanafunzi katika shule za Sekondari Pevu dhidi ya hujuma na kuingiliwa kisiasa.

Akizungumza katika Shule ya Sekondari ya Chebisaas Boys’ Ijumaa, Januari 9, 2026 baada ya kutangaza rasmi matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) 2025, Bw Ogamba aliwakosoa vikali wanasiasa kadhaa akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akiwalaumu kwa kujaribu kuhujumu mchakato wa wanafunzi kujiunga na Sekondari Pevu kwa maslahi ya kisiasa.

“Hatutakaa kimya na kuruhusu wanasiasa kuingiza siasa zisizo na maana katika sekta ya elimu,” alisema Bw Ogamba.

“Masuala ya elimu yaachwe kwa wataalamu. Nawahimiza wanasiasa hawa warudi kwenye kamusi wajifunze maana ya neno ‘kitaifa’.”

Kauli yake ilifuatia mjadala unaoendelea kuhusu uteuzi wa wanafunzi 1.1 milioni waliomaliza Sekondari Msingi mwaka jana kujiunga na Sekondari Pevu.

Kumekuwa na ushindani mkali wa nafasi katika shule za kitaifa, ambapo shule kama Alliance High School na Kenya High School zilipokea maombi zaidi ya 20,000 kila moja ilhali zina nafasi takribani 500 pekee.

Bw Gachagua amedai kuwa “wageni” wamechukua nafasi nyingi katika shule bora zilizo eneo la Mlima Kenya kwa hasara ya wanafunzi wa eneo hilo, madai ambayo aliendelea kuyatetea jana.