Onyo madaktari feki wakiongezeka TikTok
KATIKA zama hizi za kidijitali, mitandao ya kijamii kama TikTok imegeuka kuwa jukwaa maarufu kwa vijana kutafuta taarifa mbalimbali ikiwemo kuhusu afya.
Hata hivyo, hali hii imezua hofu kubwa miongoni mwa wataalamu wa afya, kwani inaibuka kuwa wengi wanaojitambulisha kama “madaktari” kwenye TikTok si wataalamu halisi wa tiba.
Wengi wao hawajasajiliwa wala hawana mafunzo rasmi ya tiba, lakini wanatoa ushauri wa kiafya kwa umma hali inayohatarisha maisha ya watu.
Imebainika kuwa baadhi ya watumiaji wa TikTok huvaa koti jeupe la daktari, hujiita ‘Daktari’, na hata kuvaa vifaa vya kazi ili kujisawiri kama wataalamu.
Kwa kutumia mbinu hizi wanajipatia wafuasi maelfu, hususan wanawake wanaotafuta msaada kuhusu matatizo ya uzazi, homoni, na magonjwa ya zinaa.
Uchunguzi uligundua kuwa baadhi ya “madaktari” hawa hulipisha huduma zao. Kwa mfano, mmoja huomba Sh100 kwa mashauriano ya mtandaoni, huku mwingine akidai kuwa ni mtaalamu wa masuala ya uzazi, lakini hakuna rekodi zake katika sajili ya madaktari nchini.
Hii ni kinyume na sheria ya Kenya, inayohitaji kila daktari awe amesajiliwa na Baraza la Madaktari na Madaktari wa Meno (KMPDC).
Baadhi ya wagonjwa wamejikuta wakitumia matibabu yasiyofaa baada ya kufuata ushauri wa mitandaoni. Mfano mmoja wa kusikitisha ni mwanamke aliyesema alianza kujitibu dalili zake za kisukari baada ya “kugundua” kupitia TikTok. Ingawa alihisi nafuu, hakupata uthibitisho wa kitaalamu na huenda alichelewesha matibabu sahihi.
Mkurugenzi Mkuu wa KMPDC, Dkt David Kariuki, alieleza kuwa hadi sasa hawajapokea malalamishi rasmi kuhusu watu wanaojifanya madaktari kwenye mitandao ya kijamii.
Alikiri kuwa ni vigumu kuwadhibiti kwani mara nyingi hawajulikani walipo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kujitambulisha kama daktari bila mafunzo rasmi ni kosa la jinai. KMPDC inahimiza umma kuthibitisha uhalali wa daktari kupitia tovuti yao au kwa kutuma ujumbe mfupi kwa nambari 2057.
Kupitia Sheria ya Afya Dijitali iliyoanzishwa mwaka 2023, serikali inalenga kudhibiti utoaji wa huduma za afya mtandaoni. Sheria hiyo inasema kuwa huduma zote za afya dijitali lazima zitekelezwe na watoa huduma waliopata leseni halali kutoka kwa taasisi husika.
Hii inalenga kuzuia watu wasio na taaluma ya tiba kueneza taarifa potofu ambazo zinaweza kusababisha madhara kwa watumiaji wa huduma.
Victor Ndede wa Amnesty International alionya kuwa taarifa za afya ni kati ya data nyeti zaidi. Alieleza kuwa watu wanaoanika dalili au historia ya matibabu kupitia TikTok wako hatarini sana kwa kuwa taarifa hizi zinaweza kuhifadhiwa au kutumiwa vibaya na wale wasio waaminifu.
Dkt Dennis Miskella wa chama cha madaktari (KMPDU) alihimiza serikali na taasisi za udhibiti kuchukua hatua kali dhidi ya matapeli wa mtandaoni.
Alieleza kuwa hata watoa huduma halali wa afya wanapaswa kupewa mafunzo kuhusu maadili ya mitandao ya kijamii ili kuepuka ukiukaji wa haki za wagonjwa.
Ingawa TikTok inaweza kuwa chanzo cha msaada wa haraka kwa watu wanaotafuta majibu kuhusu afya zao, ni muhimu kuelewa kuwa sio kila mtu aliyevaa koti jeupe ni daktari.
Umma unapaswa kuwa macho, kuthibitisha taarifa, na kuepuka kujitibu bila ushauri wa kitaalamu. Serikali nayo inapaswa kuchukua jukumu la kudhibiti maudhui ya afya mitandaoni ili kulinda maisha ya wananchi wake.
“Sio kila mtu mwenye koti jeupe ni daktari, hata wanachinja wanyama huvaa makoti meupe,” anasema Dkt Miskella.