Habari

Pasaka ya dhiki

April 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER NGARE

SIKUKUU ya Pasaka inaanza Ijumaa dunia yote ikiwa imejaa dhiki, majonzi na maombolezo kutokana na virusi vya corona.

Janga hili hata hivyo linatoa picha halisi ya huzuni ya Pasaka, ambayo ni ukumbusho wa kifo na ufufuo wa mwasisi wa Ukristo, Yesu Kristo.

Wakati huo zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, wafuasi wake Yesu walikuwa wamejaa dhiki na majonzi, kinyume na jinsi Wakristo wa siku hizi wamekuwa wakiadhimisha Pasaka kwa anasa, badala ya kutafakari maana halisi ya Yesu kujitoa uhai kama inavyoelezwa kwenye Biblia.

Kufikia jana zaidi ya watu milioni moja na laki tano duniani walikuwa wamethibitishwa kuugua virusi vya corona, ambavyo vilichipuka nchini China mnamo Desemba mwaka jana. Wengine zaidi ya elfu 90 walikuwa wamefariki.

Hapa Kenya idadi ya maambukizi yaliyothibitishwa iliongezeka hadi watu 184 jana, kulingana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Nchini Amerika pekee, watu zaidi ya milioni 435 wanaugua huku Italia ikiwa imepoteza watu elfu 17 kwa maradhi haya ambayo yamesambaa katika mataifa 209 kote duniani.

Kwa hofu ya watu zaidi kuambukizwa, mataifa mengi yameweka marufuku ya kutotoka nyumbani, kusafiri nje ya maeneo fulani, safari za ndege kusimamishwa, mipaka ya mataifa kufungwa na watu kukatazwa kukusanyika.

Hapa Kenya, wakazi wa kaunti za Nairobi, Kilifi, Kwale na Mombasa hawataweza kusafiri kuungana na familia zao kwa ajili ya kusherehekea Pasaka kama ambavyo imekuwa kawaida kila mwaka.

Hii ni baada ya serikali kuweka marufuku ya kuingia na kutoka kaunti hizo zinazoongoza kwa idadi ya watu waliothibitishwa kuugua virusi vya corona.

Mwaka huu makanisa, ambayo kwa kawaida hujaa watu kwa ibada ya Pasaka, yatakuwa mahame, waumini wakilazimika kufuatilia mahubiri kwenye televisheni, redioni na intaneti.

Hii ni baada ya serikali kupiga marufuku shughuli zote za kidini makanisani na misikitini katika juhudi za kuzuia watu kukongamana mahala pamoja.

Pia ibada ya ‘Njia ya Msalaba” ambapo Wakristo hutembea barabarani wakiigiza safari ya Yesu kuelekelea Yerusalemu kabla ya kusulubiwa haitafanyika.

Safari za mashambani na maeneo ya starehe nazo zimezimwa mwaka huu. Kwa kawaida wakati wa sherehe za Pasaka, wakazi wengi wa mijini husafiri mashambani kujumuika na jamaa zao. Lakini mwaka huu itabidi wengi kuadhimisha ndani ya nyumba zao mijini.

Kutokana na marufuku hayo ya kusafiri, watu wa bara pia hawatakuwa na shamrashamra zao za kawaida za kusafiri Pwani kujivinjari kila Pasaka inapofika.

Wahudumu wa matatu nao wanaomboleza. Pasaka huwa msimu wa mavuno ya pesa kwa wamiliki wa magari ya umma, madereva na makodkta kutokana na idadi kubwa ya wasafiri na kuongezeka kwa nauli.

Lakini mwaka huu magari mengi yamesimamisha shughuli kutokana na marufuku ya usafiri.

Pasaka pia imekuwa msimu wa sherehe za kila aina yakiwemo mapochopocho, kubugia pombe, kusakata densi, kuzuru maeneo ya kitalii miongoni mwa aina nyingine za anasa.

Sikukuu ya mwaka huu imewadia wakati ambao kuna kafyu kote nchini inayokataza watu kutoka manyumbani mwao usiku, wakati ambao miaka ya awali wengi huwa nje vilabuni wakiburudika.

Pigo jingine ni kwa waraibu wa pombe kwani baa zote zimefungwa, hali ambayo itawafanya kuona tofauti kubwa na jinsi walivyozoea kusherehekea.

Mashabiki wa soka ambao huwa na muda wa kufuatilia ligi za Uropa kwenye televisheni pia watakuwa na upweke kwani michezo yote imepigwa breki na janga la corona.

Sikukuu ya mwaka huu pia haitakuwa na jamaa na marafiki kutembeleana na kuandaa karamu kwani Wizara ya Afya na wataalamu wanashauri watu kukaa manyumbani mwao ili kuzuia kusambaza ama kuambukizwa virusi hivyo.

Watu walio na wapenzi pia wamepata pigo, ikizingatiwa ushauri kwa watu kuepuka kukumbatiana na kupigana mabusu, pamoja na safari kuzimwa. Aidha, watu wanalazimika kuvaa maski kila mara, jambo ambalo ni kikwazo kwa busu.

Wakati wa Pasaka huwa ni kipindi cha mazuri kwa wafanyibiashara hasa wa maduka makubwa, ambao hupata wateja wengi, sawa na wauzaji nyama, pombe, vinywaji na hata wachuuzi.

Huu pia huwa msimu wa vinono kwa wenye hoteli na mikahawa.

Lakini mwaka huu wateja wamepungua na watu wengi hawana pesa za kutumia kwenye burudani baada ya maelfu kusimamishwa kazi, kukosa kulipwa mishahara na biashara kuzorota.

Kwa sasa wengi wana haja ya kupata chakula cha kawaida na mahitaji mengine ya kimsingi kuliko anasa.

Covid-19 imegeuza Pasaka kuwa dhiki.