Habari

Pigo kwa Gavana baada ya mahakama kumpokonya ushindi

February 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BARACK ODUOR

GAVANA wa Homa Bay, Cyprian Awiti, Jumanne alipata pigo baada ya Mahakama Kuu kubatilisha ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Jaji Joseph Karanja aliamua kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikuandaa uchaguzi huru na wa haki ambao Bw Awiti alitangazwa mshindi.

Amekuwa gavana wa pili kupoteza kiti chake baada ya Mahakama Kuu ya Garissa kubatilisha ushindi wa Gavana wa Wajir Mohamed Abdi ambaye tayari amekata rufaa. Hapo jana, Bw Awiti pia alisema atakata rufaa.

Jaji Karanja alisema kulikuwa na matokeo mara mbili ya uchaguzi wa kiti cha ugavana cha Homa Bay ambayo yaliwasilishwa kortini na mawakili wa mlalamishi Oyugi Magwanga na mawakili wa IEBC.

Bw Cyprian Awiti (kulia) akihutubia wanahabari Februari 18, 2018 kuhusu kuwajengea wakazi wa Homa Bay makazi ya bei nafuu. Hakujua kwamba siku mbili baadaye, Februari 20, 2018, angevuliwa ugavana na makahama. Picha/ Barack Oduor

“Kulikuwa na fomu mbili tofauti kutoka kwa IEBC na walishindwa kuthibitishia mahakama zilizokuwa na matokeo halisi,” jaji alisema.

“IEBC ilishindwa kuthibitishia mahakama kwamba stakabadhi za Bw Magwanga zilikuwa ghushi,” alisema Jaji Karanja.

Aidha, alisema tume ilikosea na kushindwa katika majukumu yake na kwamba ni lazima iwajibike kwa makosa yake.

Katika uamuzi wake, Jaji alilaumu maafisa wa uchaguzi wa IEBC kwa kushindwa kueleza makosa yaliyopatikana katika fomu zao akisema kila shughuli huwa na matokeo na wasimamizi wa uchaguzi wa tume walishindwa kuelezea makosa katika fomu zao.

Bw Oyugi Magwanga ajumuika na wafuasi wake kushuhudia kura za ugavana wa Homa Bay kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 zikihesabiwa upya mahakamani Februari 18, 2018. Picha/ Barack Oduor

Kura zilibadilishwa

Jaji Karanja alisema IEBC haikujali kueleza kwa nini idadi ya kura katika fomu zake ilibadilishwa, fomu ambazo hazikuwa zimeandikwa chochote na masanduku ya kura ambayo hayakuwa au yaliyokuwa na vibandiko vilivyofunguliwa.

Jaji pia aliwalaumu mashahidi wa Bw Magwanga kwa kutokuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu madai ya hongo. Alitaja video iliyowasilisha kortini kama ushahidi wa madai ya ghasia na vitisho akisema haingetosha kuthibitisha Bw Awiti alishirikiana na tume kuiba kura.

Mbunge wa zamani wa Kasipul Bw Oyugi Magwana aungana na wafuasi wake Februari 20, 2018 mjini Homa Bay kusherehekea uamuzi wa maahakama wa kufutilia mbali ushindi wa Cyprian Awiti. Picha/ Barack Oduor

“Ushahidi wa video na madai mengine yaliyowasilishwa na mashahidi wa Mugwanga haukuweza kuthibitisha kwamba Bw Awiti alihusika na makosa yaliyodaiwa,” alisema Jaji.

IEBC ilimtangaza Awiti mshindi kwa kura 210,173 na Mugwanga akiwa wa pili kwa kura 189,060.

Kwenye kesi yake, Mugwanga ambaye alikuwa mbunge wa Kaspul, alisema alikuwa na kituo chake cha kujumlisha matokeo kilichoonyesha kwamba alishinda kwa kura 224,863 dhidi ya 174,235 za Bw Awiti.