Habari

Polisi wachunguza sakata ya bastola kati ya Babu Owino na Alai

Na NDUBI MOTURI January 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

POLISI jijini Nairobi wanafanya uchunguzi kuhusu mabishano yaliyotokea Jumamosi, Januari 03, 2026 alasiri kati ya Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, na Diwani wa Wadi ya Kileleshwa, Robert Alai, ambapo inadaiwa kuwa diwani huyo alitoa bastola.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilimani, Bi Patricia Yegon, alisema viongozi hao wawili tayari wameandikisha taarifa zao na polisi watawahoji wateja pamoja na wafanyakazi wa mkahawa waliokutana ili kubaini ukweli wa kilichotokea.

“Kwa kuzingatia ushahidi uliopo—ikiwemo kupitia kanda za CCTV na mahojiano na wote waliokuwapo—tunatarajia kubaini ni nani hasa alitenda kosa. Bila kujali cheo cha mtu, tutachukua hatua zinazofaa,” Bi Yegon aliwaambia waandishi wa habari katika mkahawa huo ulio Kilimani.

Katika taarifa yake, Bw Owino alimshutumu Bw Alai kwa kumvamia kwa silaha wakati wa mkutano mfupi katika mkahawa huo maarufu jijini.

Hata hivyo, Bw Alai amekanusha madai hayo akisema tayari ameripoti tukio hilo kwa polisi na atatoa maelezo yake “wakati mwafaka”.

Kwa mujibu wa Bw Owino, tukio hilo lilitokea Jumamosi alasiri baada ya kuhudhuria mkutano wa faragha na kiongozi mmoja mkuu wa kidini. Alisema alikuwa amewaachilia walinzi wake kwa mapumziko ya Krismasi, hivyo alikuwa peke yake alipofika katika mkahawa huo muda mfupi kabla ya saa kumi jioni.

Alipokuwa akiondoka, alisema alisimama kusalimia watu waliokuwa wamekaa mezani karibu, akiwemo Bw Alai. Alidai hali ilibadilika haraka baada ya diwani huyo kumlaumu  kwa kupanga mashambulizi ya mitandaoni dhidi ya mke wa Bw Alai, madai ambayo Mbunge huyo alikana vikali.

“Sijui mke wake, na sijawahi kuhusisha familia katika siasa,” alisema Bw Owino, akitaja tuhuma hizo kuwa zisizo na msingi.

Mbunge huyo alidai kuwa Bw Alai alikua mkali, “alinisukuma, akatoa bastola na kunipiga nayo kifuani na kwenye taya, yote yalishuhudiwa na wateja waliokuwapo.”

Alisema alijaribu kutuliza hali hiyo na hata kuketi kwa muda baada ya mtu wa tatu kuingilia kati. Hata hivyo, alidai kuwa muda mfupi baadaye Bw Alai alimrushia maji usoni, hali iliyovutia umati, ndipo akaondoka haraka na kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.

Bw Owino alielezea tukio hilo kama tishio la moja kwa moja kwa maisha yake, akidai ni sehemu ya njama endelevu ya vitisho vya kisiasa dhidi yake. Alirejelea tukio la awali huko Siaya wakati wa mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ambapo alidai wahuni walichochewa dhidi yake.

Hata hivyo, Bw Alai alipuuza madai hayo. Akizungumza na Taifa Leo Jumapili, alisema Mbunge huyo anaeneza uvumi.

“Ameenda kueneza uvumi kuhusu tukio hilo. Aendelee tu,” alisema. “Nitazungumza kwa kina kuhusu tukio hilo wakati unaofaa.”

Kufikia Jumapili alasiri, polisi hawakuwa wametoa taarifa rasmi kuhusu hatua za uchunguzi, ikiwemo iwapo CCTV imekaguliwa, mashahidi kuhojiwa au mashtaka kuzingatiwa.