Habari

Polisi wakamata watu 27 kanisani Changamwe wanaohusishwa na itikadi kali

Na MISHI GONGO November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI katika eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa, wanawazuilia watu 27 wakiwemo wanawake na watoto waliopatikana wamejifungia ndani ya kanisa, wakidaiwa kuhusiana na kundi la itikadi kali za kidini.

Kundi hilo lilipatikana ndani ya kanisa baada ya maafisa wa usalama kupokea taarifa kutoka kwa umma kwamba mwanamke mmoja alikuwa amewaondoa watoto wake shuleni na kuwafungia kanisani, bila kuwapa huduma za afya wala elimu.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu,Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Changamwe, Patrick Gogo, alisema maafisa wake walivamia kanisa hilo Ijumaa na Jumatatu, ambapo walifanikiwa kuwaokoa watu 27 wakiwemo wanawake saba na watoto 20 wenye umri wa kati ya miaka miwili hadi 15.

“Tulipokea taarifa kwamba mama mmoja amewaondoa watoto wake shuleni na kuwafungia kanisani. Tulipoenda huko tulipata kundi kubwa likiwa humo ndani,” alisema Bw Gogo.

Kulingana na kamanda huyo watoto hao walipatikana wakiwa katika hali ya kusikitisha, wengi wao wakiwa wamelala sakafuni bila neti za mbu.

“Tulipowakuta, walikuwa wamelala sakafuni bila neti. Tunajua eneo la Pwani lina mbu wengi, hivyo hali hiyo inawaweka hatarini kupata magonjwa,” aliongeza.

Kulingana na polisi, baadhi ya watoto hao wangefaa kuwa wakifanya majaribio ya KJSEA, lakini walizuiliwa kanisani badala ya kuwa shuleni.

“Tunachunguza kujua wamekuwa huko kwa muda gani na wamekuwa wakifanya nini,” alisema Bw Gogo.

Alisema uchunguzi wa awali ulianza Ijumaa baada ya mwanamke mmoja na watoto watatu kupatikana, kisha akawaongoza polisi kwa wengine waliokuwa kanisani humo.

Polisi wamewaita wachungaji na viongozi wa kanisa hilo kwa mahojiano, lakini hadi sasa hakuna aliyefika kutoa maelezo.

Bw Gogo aliwataka wakazi wa Mombasa kuwa makini na makundi yenye mafundisho ya kupotosha, akisisitiza umuhimu wa kufuata mafundisho ya Kikristo halisi.

“Ni kawaida waumini kulala kanisani siku za ibada kama Ijumaa, Jumamosi au Jumapili, lakini si kuficha watoto na kuwanyima elimu. Watu wajiepushe na makundi ya ajabu ili tusije tukashuhudia visa kama vya Shakahola au Kwa Binzaro,” alisema.

Watoto na wanawake waliookolewa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi Changamwe wakisubiri uchunguzi zaidi kuhusu asili ya kundi hilo.