Habari

Polisi wanyaka wasiovaa maski

April 14th, 2020 3 min read

Na WAANDISHI WETU

POLISI Jumanne walianza mara moja kukamata watu wanaotembea bila kuvalia barakoa baada ya Inspekta Jenerali, Hillary Mutyambai kutoa agizo hilo.

Bw Mutyambai alitoa amri hiyo siku chache baada ya masharti hayo kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la Serikali.

Kulingana na Bw Mutyambai, Wakenya walipewa muda wa kutosha kujizoesha kutembea na barakoa hizo wakati wowote wanapotoka nje ya nyumba zao kwa hivyo hakuna sababu ya kulegeza sharti hilo.

Haikuchukua muda mrefu kabla kubainika watu kadhaa tayari walianza kukamatwa katika mitaa mbalimbali ya Nairobi.

Kabla agizo hilo kutolewa, polisi walikuwa wakati wote wakitumia mbinu za kiungwana kukumbusha wananchi kununua barakoa wakiwakuta bila yoyote hadharani.

“Polisi wamekuwa wakishirikiana na umma kuwaomba wavae barakoa. Sasa tutapiga hatua mbele ili kuhakikisha kila mtu anajifunga barakoa. Lakini kwanza nataka kuomba Wakenya wawe wakifanya hivyo kwa hiari,” akasema Bw Mutyambai.

Alikuwa akizungumza alipopokea barakoa 200,000 za kutumiwa na polisi kutoka kwa Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) na shirika la Ahadi Kenya.

Utumiaji wa barakoa umethibitishwa kupunguza ueneaji wa virusi vya corona katika mataifa mengi duniani.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya husema hawana uwezo wa kununua barakoa hizo zinazogharimu kuanzia Sh50 kila mara kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Badala yake, wanapendekeza wapewe na serikali bila malipo.

Msemaji wa Serikali, Kanali (Mstaafu) Cyrus Oguna jana alisema serikali ingali inaendeleza mipango ya kuanza kusambaza barakoa kwa jamii zisizojiweza kifedha.

Kwa mujibu wa masharti yaliyochapishwa wiki iliyopita, mtu yeyote ambaye atapatikana nje bila barakoa atatozwa faini ya Sh20,000 au afungwe jela miezi sita.

Wananchi wengi walikuwa wakiendelea kupuuza masharti hayo mapya.

Kwa mfano, katika lokesheni ya Mukuru-Nyayo, eneobunge la Starehe, wakazi walionywa kwamba wanahatarisha maisha yao wenyewe kwa kupuuza kuvaa barakoa wakiwa mitaani.

Kando na hayo, wengi wamekuwa wakikusanyika pamoja na kupuuza masharti ya serikali.

“Katika mitaa ya mabanda ya Mukuru-Maasai, Mukuru-Hazina, Diamond na Balozi, watu wanatangamana kiholela na hawaonekani kutishika na virusi vya corona,” mwenyekiti wa mtaa wa Balozi, Bw Mohammed Hussein asema.

Hayo yalijiri wakati ambapo idadi ya maambukizi iliendelea kuongezeka nchini jana.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema kwa kipindi cha saa 24 kufikia jana, watu wanane kati ya 694 waliochunguzwa kimatibabu walipatikana kuambukizwa virusi vya corona.

Watano kati yao ni raia wa Kenya, huku watatu wakiwa raia wa Uingereza, Pakistan na Uganda. Sita kati yao walipatikana Nairobi, mmoja Siaya na mwingine Nakuru.

Mtu mwingine mmoja alithibitishwa kupona na kupelekea idadi ya waliotibiwa corona kikamilifu kufika 41.

Hata hivyo, Dkt Mwangangi alisema wale waliopona bado wataendelea kufuatiliwa kwani ilibainika katika nchi nyingine za nje, kuna watu waliopona lakini baadaye wakapatikana na virusi vya corona upya.

Nairobi ingali na idadi kubwa ya maambukizi 101, ikifuatwa na Mombasa (34), na Kilifi (10).

Wakati huo huo, wabunge jana walihalalisha hatua ya serikali ya kushusha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kupunguza bei ya bidhaa za kimsingi wakati huu ambapo Wakenya wanaokabiliwa na changamoto zinazosababishwa na janga la corona.

Walifanya hivyo kwa kupitisha ripoti ya Kamati kuhusu Sheria Mbadala iliyowasilishwa bungeni na mwanachama wa kamati hiyo Tharaka Gitonga Murugara (Mbunge wa Tharaka), kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo Gladys Shollei (Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu).

Hata hivyo, baadhi ya wabunge kama vile Kimani Ichungwa (Kikuyu), Makali Mulu (Kitui ya Kati) na Amos Kimunya (Kipipiri) walipitisha ripoti hiyo shingo upande wakidai Sh49.5 bilioni ambazo zitapotezwa kufuatia hatua hiyo zingetumiwa kuwasaidia familia masikini.

Lakini kauli zao zilipingwa na wenzao wakiongozwa na kiongozi wa wengi Aden Duale walioshikilia kuwa hatua hiyo itapelekea kupungua kwa bei ya bidhaa za kimsingi kama vile unga, maziwa na sukari, zinazotegemewa na Wakenye masikini.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini aliwataka wafanyabiashara kupunguza bei ya bidhaa kama hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwajali Wakenya wa kawaida.

Ripoti za Vincent Achuka, Sammy Kimatu, Valentine Obara na Charles Wasonga