HabariSiasa

Puuzeni madai ya mpango wa kumuua Ruto – Wabunge

June 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

BAADHI ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya Jumatatu jioni walijitokeza kupinga madai kuwa mawaziri wa kutoka eneo hilo wanapanga kumuua Naibu Rais William Ruto.

Wabunge hao walitaja madai nayo kuwa upuuzi ambao unalenga kuchochea jamii zingine nchini kutengana na Mlima Kenya, wakisema mawaziri hao hawajafanya mpango wowote wa aina hiyo.

Wakiongozwa na mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu, wa Kiambaa Paul Koinange, Gathoni Wamuchonba (Mbunge Mwanamke wa Kiambu), Maoka Maore (Igembe), Joseph Nduati (Gatanga) na Ruth Mwaniki (Kimumo), viongozi hao aidha walisema kuna njama ya kuvuruga serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, asifanye Nazi.

“Kuna juhudi za kuchochea nchi dhidi ya viongozi Wa Mlima Kenya na Rais mwenyewe,” Bw Wambugu akasema, akishangaa kwa nini viongozi wa maeneo mengine nchini wanapokutana hawaambiwi kuwa wana mipango mingine.

“Tuache kushuku kila kitu na kuweka siasa kila mahali. Watu waache kudhani kuwa wengine wakikutana wanawapangia mabaya tu,” Bi Wamuchomba naye akasema.

Bw Koinange aidha alisema kuwa “Naibu Rais ni wa pili kwa wanaolindwa zaidi Kenya hivyo aache kuwapotosha Wakenya. Ukiwa na vita vya kisiasa ama chama vilete kwa wanasiasa, si kwa mawaziri. Huu ni mpango wa kuvuruga ajenda za maendeleo za Rais.”

Wabunge hao walisema wako nyuma ya mawaziri hao kwa kuwa ndio wanasukuma ajenda za maendeleo serikalini kwa niaba ya eneo la Mlima Kenya.

“Kuwapiga mawaziri kutoka eneo letu ni kutupiga na kupiga wakazi wetu,” akasema Bw Ngunjiri