Habari

Raia washauriwa kufungua milango wakati wa sensa

August 1st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Kitaifa la Takwimu (KNBS) limetoa wito kwa Wakenya kuwakaribisha maafisa wake nyumbani ili wachukua habari kuhusu familia zao wakati wa shughuli ya mwaka 2019 ya kuhesabu watu, maarufu kama sensa.

Akiongea jijini Nairobi Alhamisi alipozindua msafara wa malori ya kutoa uhamisisho kuhusu shughuli hiyo katika kaunti zote 47, Katibu wa Wizara ya Fedha anayesimamia Idara ya Mipango Saitoti Torome alisema maafisa hao watakuwa wakiandamana na maafisa wa usalama.

“Tunawaomba Wakenya wote kuwapokea maafisa wa takwimu (enumerators) kutoka KNBS mnamo Agosti 24 na 25. Watakuwa wakiandamana na maafisa wa usalama nyakati zote kwa sababu shughuli hiyo itaendeshwa usiku,” akasema Bw Torome.

Bw Torome alikariri kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa sababu matokea yake yataisaidia serikali kuratibu mipango yake ya maendeleo barabara.

“Sensa ni shughuli muhimu itakayotumiwa kukusanya data ambayo itatumiwa na serikali kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo yaliyoko kwenye Ruwaza ya Maendeleo ya 2030, Malengo Endelevu ya Maendeleo yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa (SDG) na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo za Serikali ya Jubilee,” akaeleza.

Huku akiwahimiza Wakenya kujiandaa, Bw Torome ameongeza kuwa takwimu zitakazopatikana kutokana na sensa zitaisaidia serikali kujua rasilimali zinazohitajika katika sekta za elimu, afya, maji na usafi, nyumba, miundombinu na nyinginezo katika eneo fulani.

“Tunahitaji kujua idadi ya watu ili tupange bajeti ya miradi kama hii,” akasema.

Mipango yaendelea

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa KNBS Zachary Mwangi amewahakikishia Wakenya kwamba mipango yote ya maandalizi ya sensa inaendelea ilivyopangwa.

“Tungependa kuwahakikishia Wakenya kwamba mipango yote ya sense ya 2019 inaendelea ilivyopangwa. Idara zote za serikali zinashirikiana kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaendelea ilivyopangwa bila tashwishi,” akasema.

Bw Mwangi akaongeza: “Mafunzo kwa maafisa watakaoendesha sensa yanaendelea na mitambo ya kukusanya data inasambazwa katika vituo mbalimbali na shughuli hiyo inakamilika wiki hii.”

Makundi ya msafara wa KNBS wyatawahamisha wananchi kuhusu umuhimu wa shughuli ya sensa, sio tu kwa taifa bali kwa kila mwananchi.

Jumbe zitakazotolewa na misafara hiyo haswa zitalenga wakuu wa nyumba ambao ndio watawaalika maafisa wa shirika hilo na kuwapa habari sahihi.

Misafara hiyo itazunguka kote nchini hasa katika maeneo yenye watu wengi kama vile masoko ili kuwapa maelezo muhimu kuhusu sensa na kujibu maswali mbalimbali kuhusu shughuli hiyo, amesema Bw Mwangi.