Habari

Raila anyakua kazi ya Ruto

February 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amezidi kuibua maswali kuhusu mamlaka aliyo nayo katika serikali inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Jumapili alipoongoza mkutano wa hadhara kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) katika Kaunti ya Garissa, Bw Odinga alijitwika majukumu ambayo kwa kawaida yanafaa yatekelezwe na viongozi wakuu serikalini, hasa Naibu Rais William Ruto.

Waziri huyo mkuu wa zamani alijitosa katika mdahalo unaohusu kuhamishwa kwa walimu wasio wenye asili ya maeneo ya Kaskazini Mashariki kufuatia mashambulio ya kigaidi yaliyokuwa yakiwalenga.

Katika hotuba yake, aliwaahidi wakazi wa Garissa kwamba serikali itatatua suala hilo na mabadiliko yataonekana hivi karibuni.

“Hakuna kitu kichungu zaidi kama watoto kwenda shuleni na kupata hakuna walimu. Hili ni jambo la kusikitisha na ni lazima tupate suluhu. Lazima tulete walimu hapa,” akasema.

Aliongeza kwamba alikuwa tayari amejadiliana na Rais Kenyatta, kwa hivyo, kuna uhakika serikali itachukua hatua.

Alisema inafaa vijana waliopata alama za C- na D+ katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) kutoka kaunti zilizo Kaskazini Mashariki waruhusiwe kujiunga na taasisi za mafunzo ya walimu.

“Nimeongea na Rais Uhuru kabla nije hapa… na narudi kuongea naye tena. Wiki ijayo, mtaona matangazo kisha walimu wataletwa hapa,” akasema.

Mbali na hayo, Bw Odinga alitoa ahadi kuhusu masuala ya miundomsingi na usalama katika eneo hilo linalopakana na Somalia. Kulingana naye, mashambulio ya kigaidi yanayofanyika barabarani Kaskazini Mashariki, yanafaulu kwa sababu ya barabara mbovu ambazo zinatoa nafasi kwa magaidi kushambulia magari kila mara.

Alisema, alipokuwa waziri mkuu, alitoa mchango mkubwa katika mpango wa kujenga barabara inayotoka Garissa kupitia Wajir hadi Mandera, na akaongeza kuwa serikali itakamilisha mradi huo.

“Mimi ndiye niliyechora barabara za Garissa kupitia Wajir mpaka Mandera. Hiyo barabara itajengwa. Tunataka kuona eneo hili linafunguliwa. Tukifikisha lami kule Mandera, mambo haya ya ujambazi na ujangili yatakoma,” akasema.

Katika hotuba za awali, Dkt Ruto alisema jukumu la kutangaza au kuzindua miradi ya serikali ni lake kama naibu rais akisema kuwa huwa anapokea mshahara kufanya kazi hiyo.

Lakini wiki chache zilizopita, Rais Kenyatta alishangaza wengi alipokemea watu ambao hakuwataja, akisema wamemsaliti licha ya kuwa aliwaamini na kuwapa jukumu la kuendesha miradi mikuu ya serikali yake.

Tangu Bw Odinga alipokubali kushirikiana na Rais Kenyatta kupitia kwa handsheki mwaka wa 2018, hadhi yake imepanda sana serikalini.

Ahadi zake za Jumapili zimeongeza orodha ya matukio yanayomfanya kuonekana kama kiongozi mwenye mamlaka makubwa serikalini. Matukio mengine yanahusu ulinzi mkubwa anaopewa, ijapokuwa duru zingine hudai ulinzi huo unatokana na mamlaka yake kama Balozi wa Miundomsingi katika Muungano wa Afrika.

Vilevile, kumekuwa na wakati ambapo mawaziri serikalini walikuwa wakimtembelea afisini mwake kumwarifu kuhusu shughuli za serikali kuu.

Wandani wa Naibu Rais walio katika mrengo wa Tangatanga, humlaumu Bw Odinga wakidai alitumia handsheki kujiingiza serikalini kupitia mlango wa nyuma na kuvuruga Chama cha Jubilee.

Jumapili, Dkt Ruto na kikosi chake waliendelea kukemea mikutano ya BBI wakisema inatumiwa kugawanya nchi na kusababisha taharuki katika jamii.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria ambaye aliandamana na Naibu Rais kwa harambee ya Waislamu katika uwanja wa michezo wa Embu, alisema bunge litaanza kuchunguza ufadhili wa mikutano hiyo.

“Wanaita wengine wafisadi ilhali kile kinachofanyika katika mikutano ya BBI ndiyo ufisadi zaidi kwa kuwa bunge halijapitisha hata shilingi moja kufadhili mikutano hiyo. Wanaochukua pesa za umma, mtajikuta bungeni kujibu maswali,” akasema.

Rais Kenyatta amekuwa akitoa wito kwa viongozi wote kuunga mkono shughuli za BBI, akisema lengo ni kuleta umoja nchini. Wikendi ijayo, mkutano wa BBI unatarajiwa kufanyika katika Kaunti ya Meru ambapo waandalizi wanasema wamemualika pia Rais Kenyatta na Dkt Ruto.