Habari

Raila asukumwa awe Rais

August 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WAANDISHI WETU

SHINIKIZO za kumtaka kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga awanie urais zimeongezeka licha ya kigogo huyo wa siasa nchini kusalia kimya kuhusu malengo yake ya 2022.

Mjadala kuhusu hatima yake kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao ulitokota Jumapili, baada ya Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe, kudokeza kuwa kuna mipango serikalini ya kumkweza Bw Odinga hadi Ikulu ili aongoze kwa miaka mitano kuanzia 2022.

Katika mahojiano kwenye runinga, Bw Murathe ambaye ni mmoja wa wandani wakubwa wa Rais Uhuru Kenyatta alitaja mipango hiyo kuwa sawa na ilivyofanyika Afrika Kusini wakati marehemu Nelson Mandela alitunukiwa nafasi ya kuongoza ili atoe mwelekeo wa uongozi bora.

“Tunaamini wakati umefika kwa Wakenya kumtuza Raila Amollo Odinga kwa kujitolea kwake kwa miaka mingi. Wakenya wana deni lake. Ni kama vile Mandela. Lakini tungependa kumwambia awe rais wa mpito ambaye atawezesha vijana kuingia uongozini ifikapo 2027,” akaeleza.

Ingawa Bw Odinga hukataa kuelezea iwapo anapanga kuwania urais, Bw Murathe alisisitiza ni wazi atakuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho.

Matamshi yake yaliibua hisia mseto kutoka kwa viongozi na wafuasi wa Bw Odinga.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli, aliunga mkono kauli ya Bw Murathe.

Akizungumza nyumbani kwake Kajiado ambapo alitarajiwa kukutana na viongozi mbalimbali akiwemo Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, katibu huyo alisema Bw Odinga ndiye anastahili zaidi kumrithi Rais Kenyatta.

Suala kuhusu urithi wa Rais Kenyatta ifikapo 2022 limekuwa likiibua msisimko katika ulingo wa kisiasa, hasa ikizingatiwa kwamba uhusiano wake na naibu wake, Dkt William Ruto umesambaratika ikilinganishwa na wakati walipoingia mamlakani 2013.

Wakati huo, iliaminika Rais angemsaidia Dkt Ruto kuingia Ikulu baada ya kuongoza kwa mihula miwili.

Bw Atwoli alieleza kwamba, ingawa kuna wanasiasa wengi ambao wana uwezo wa kuongoza nchi, 2022 inastahili kuachiwa Bw Odinga ili asafishe mandhari ya kisiasa na kiuchumi.

Alisisitiza kuwa balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU) anaweza kushinda urais mapema asubuhi kama atakubali kuwania kiti hicho.

Wiki chache zilizopita, Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw Oburu Oginga ambaye ni kakake Bw Odinga, alikuwa amedai atasaidiwa na watu wenye ushawishi serikalini kuingia mamlakani.

Kulingana naye, kikundi hicho cha watu almaarufu kama ‘system’ ndicho kilikuwa kikwazo kwa Bw Odinga kuingia katika Ikulu miaka iliyopita, lakini sasa amepata baraka zao kwa kushirikiana na Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Muungano wa jamii za Gikuyu, Embu na Ameru (Gema) kupitia mwenyekiti wake Askofu Mstaafu Lawi Imathiu ulisema wananchi ndio wataamua atakayekuwa rais.

“Uwanja uko wazi kwa wote na kazi yetu ni kuwasikiza na kuwafuatilia na hatimaye tutafanya uamuzi wetu wa kibinafsi kama wapiga kura,” akasema.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth na ambaye anapendekezwa na baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya arithi usemaji wa kijamii kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta alisema watasubiri tangazo kutoka kwa Rais Kenyatta kuhusu anayemtaka awe mrithi wake.

“Ikiwa Rais kwa busara yake ataonelea atuongoze kwa Bw Odinga, basi sisi tutatii,” akasema Kenneth.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau alisisitiza kuwa matamshi ya Bw Murathe yanafaa kuchukuliwa kwa uzito.

Hata hivyo, Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro, aliye mwandani wa Dkt Ruto alipuuzilia mbali dhana kuwa Ikulu inamwandaa Bw Odinga kuwa rais.

Katika eneo la Nyanza ambayo ngome kuu ya kisiasa ya Bw Odinga, Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alisema Bw Odinga ndiye mwanasiasa wa kipekee nchini ambaye anaweza kuendeleza kazi iliyoanzishwa na Rais Kenyatta.

Lakini baadhi ya wakazi eneo hilo walimtaka Bw Odinga kujihadhari na ahadi kuhusu urais, kwani amewahi kuchezewa shere katika tawala zilizopita za marehemu Daniel arap Moi na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Mwenyekiti wa vuguvugu la wakazi wa Kisumu, Bw Audi Ogada, alisema ni wazi Bw Odinga anastahili kutuzwa kwa jinsi alivyojitolea kuikomboa nchi lakini asiamini ahadi anazopewa hadi zitekelezwe.

 

Ripoti za Charles Wasonga, Valentine Obara, Mwangi Muiruri na George Odiwuor