Raila awakejeli viongozi ‘bubu’ katika janga la corona
Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amekejeli viongozi waliotoweka machoni mwa umma pindi tu janga la corona lilipobisha nchini Kenya.
Matamshi yake yalionekana kuelekezwa kwa wanasiasa ambao, kabla ya virusi vya corona kuanza kuenea humu nchini, walikuwa wakionekana kila pembe ya nchi wakiendeleza kampeni kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Viongozi wengi wa mirengo yote ya kisiasa hawajaonekana hadharani kwa takriban mwezi mmoja sasa, huku wachache wao wakionekana tu katika mitandao ya kijamii na wengine wakitumia janga hili kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Bw Odinga jana alisema huu si wakati wa wanasiasa na viongozi kukaa nyumbani huku wananchi wakiwa na mahitaji mengi kutokana na janga la corona.
Vilevile, alisema huu si wakati wa siasa bali wa ushirikiano kusaidia kupambana na corona.
“Janga hili la corona limewaletea wananchi shida nyingi sana. Biashara zimeporomoka na viongozi tunafaa kuacha siasa, tuungane kupigana na corona,” alisema katika mahojiano kwenye kituo cha redio cha Citizen jana asubuni.
Alikejeli hasa wanasiasa waliokuwa katika mstari wa mbele kutoa mamilioni ya pesa kwenye harambee na makanisani kabla ya corona kuripotiwa nchini ilhali sasa wamenyamaza.
“Wanasiasa wameenda chini ya maji, hawasaidii Wakenya. Wamezoea siasa za kupinga wenzao. Ni wakati wa kutoa huduma kwa wananchi. Walikuwa wanatoa michango makanisani. Wanasubiri yafunguliwe ndipo waanze kutoa? Kuna watu wanaohitaji misaada kila mahali kwa sasa na ningewaomba viongozi wenzangu tuungane tuwasaidie Wakenya,” Bw Odinga alisema.
Kuhusu iwapo serikali inapaswa kutangaza amri ya kutotoka nje kabisa huku maambukizi ya corona yakiongezeka, Bw Odinga alisema hiyo inaweza kuwa hatua ya mwisho kabisa na inahitaji maandalizi kabambe kulinda raia.
“Serikali haitakuwa na chaguo. Maendeleo ni muhimu lakini maisha ni muhimu zaidi. Serikali ianze kujiandaa, ikifika wakati huo kuwe na chakula cha kutosha,” akasema.
Alieleza kuwa, kwa sasa serikali haina uwezo wa kutosha kiuchumi kusaidia kila mwananchi mwenye mahitaji endapo agizo la kutotoka nje kabisa litatolewa.
“Mitaa ya wakazi wa mapato ya chini mijini watahitaji kusaidiwa kwa chakula. Watu wa mashambani wanaweza kujitafutia, mijini kuna changamoto,” alisema.
Balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU) alisema agizo hilo lilipitishwa katika nchi kama Rwanda kwa sababu ukubwa wake unaweza kufananishwa na mkoa mmoja wa Kenya, na Afrika Kusini ambayo imestawi kiuchumi ikilinganishwa na Kenya.
Wakati huo huo, alitetea hatua ya serikali kuagiza mahindi kutoka nje ya nchi na kuwataka watu waache kuingiza siasa katika suala hilo.
Aliwataka wakulima wajitolee kuuza mahindi badala ya kuyaficha kisha kulalamika wakati serikali inapoagiza kutoka nje.
“Serikali lazima imefanya utafiti. Wale walio na mahindi hawajazuiwa kuuza. Ninaunga hatua ya Waziri Peter Munya kwa sababu tathmini inaonyesha hakuna chakula cha kutosha,” alisema.
Serikali imetangaza kuwa itatoa vibali kwa wafanyabiashara wa humu nchini kuagiza mahindi ya kima cha Sh2 bilioni ili kulinda nchi dhidi ya uhaba wa chakula msimu huu wa janga la corona.
Kuhusu mipango ya kurekebisha katiba, Bw Odinga alikariri kwamba mchakato huo haujasitishwa.
Alisema jopo lililotwikwa jukumu la kuendesha mchakato huo lingali linaendelea na shughuli zake, akaeleza matumaini kwamba corona itatuondokea hivi karibuni na hali ya kawaida kurejelewa.
“Reggae haijasimama, inaendelea, itakuja juu tena. Kuna watu waliodai kuwa wamesimamisha reggae, corona sio mtu,” alisema. Hata hivyo alikiri kwamba janga hili limeathiri kasi ya mpango huo.
“Corona imetutoa pumzi kidogo, tutabadilisha mbinu. Tulikuwa karibu tumalize, ripoti inaendelea kuandikwa, kazi inaendelea, tukirudi, tutapeleka mapendekezo yanapohitajika, serikali kuu, bunge na yanayohitaji kura ya maamuzi yapelekwe kwa wananchi,” alisema. Waziri huyo mkuu wa zamani alisema bado kuna muda wa kufanya referenda.
“Wakati upo, tuna hakika itafanyika, corona haitaendelea kwa muda mrefu,” alisem