‘Raila bado anao ushawishi mkubwa eneo la Magharibi’
BARACK ODUOR na CHARLES WASONGA
MBUNGE mteule Godfrey Osotsi Jumamosi alishikilia kuwa kiongozi wa NASA Raila Odinga bado ana ushawishi mkubwa katika eneo la magharibi mwa Kenya licha ya tofauti kati yake na vinara wenza Moses Wetang’ula na Musalia Mudavadi.
Wawili hao wamedai Bw Odinga aliwasaliti kwa kubuni ushirikiano na Rais Uhuru Kenyatta bila kisiri bila kuwajulisha licha wao kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Ushawishi wa Raila Odinga katika mkoa wa magharibi bado ni mkubwa japokuwa ndugu zangu Moses Wetang’ula na Musalia Mudavadi wameamua kumpinga kwa kuhusiana na mwafaka wake wa Rais Kenya. Watu wa eneo hilo bado wanamuenzi zaidi,” Bw Osotsi akasema.
Mbunge huyo wa chama cha Amani National Congress (ANC) alisema hayo jana katika hafla ya kuchanga pesa za kuisadia Kanisa la Chang Roho Maler, katika kijiji cha Gul Kagembe, eneo bunge la Rangwe, kaunti ya Homa Bay.
Kauli yake inajiri wiki moja baada ya Mabw Mudavadi na Wetang’ula kuwaitaka jamii ya Waluhya kutokiunga mkono chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Walidai Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa chama hicho ameisaliti jamii hiyo kwa kuchochoea kuondolewa kwa Bw Wetang’ula kama kiongozi wa wachache katika seneti.