Habari

Raila chaguo la Mlimani?

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

DICKENS WASONGA na MARY WANGARI

WAZEE wa jamii ya Agikuyu, Jumamosi walimwidhinisha kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga na kuahidi kutembea pamoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Kundi la wazee zaidi ya 700, likiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu, Mzee Wachira Kiago jana lilitangaza azma ya kufanya kazi pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu na jamii ya Waluo kwa jumla.

Katika hafla hiyo iliyoandaliwa nyumbani kwake Bw Odinga, eneo la Kang’o ka Jaramogi mjini Bondo, na kuhudhuriwa na wanasiasa mashuhuri, wazee hao wa eneo la Mlima Kenya walimkabidhi Bw Odinga zawadi mbalimbali kama ishara ya mkataba baina ya jamii ya Agikuyu na jamii ya Waluo.

Aidha, wazee hao walitahadharisha jamii hizo mbili dhidi ya kukiuka mkataba huo, wakionya kuwa watakaoenda kinyume watapata madhara ambayo hayakubainishwa.

“Hatuandiki mkataba wetu katika kijipande cha karatasi lakini tumefanya matambiko ya kitamaduni yenye uzito ili kuashiria kile tunamaanisha,” alisema mwenyekiti wa baraza hilo.

Bw Kiago alieleza kuwa wazee kutoka jamii ya Agikuyu na jamii ya Waluo walikuwa wamefanya mkataba utakaowawezesha kufanya kazi kwa pamoja, ambapo baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya waliahidi kumaliza uhasama wa kisiasa ambao kwa muda mrefu umetenganisha jamii hizo mbili.

Kulingana na mwenyekiti huyo, hafla hiyo ni kilele cha msururu wa mikutano ambayo imekuwa ikifanyika kati ya jamii hizo mbili kwa lengo la kuzileta pamoja na kuimarisha handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM.

Bw Odinga alikosa kuhudhuria ibada ya maombi ya kitaifa iliyoandaliwa ikulu na kuhudhuriwa na Kiongozi wa Taifa na Naibu wake Dkt William Ruto, na badala yake kuwapokea wazee hao katika ngome yake.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanasiasa kadhaa maarufu kutoka eneo la Mlima Kenya wakiwemo aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Mbunge Maina Kamanda, Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni na Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyeri Dkt Caroline Karugu, aliyemkabidhi Bw Odinga zawadi kutoka kwa wazee hao.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Bw Odinga alichapisha picha kuhusu hafla hiyo ambapo wazee wa jamii ya Agikuyu walionekana wamevalia magwanda yao ya kitamaduni pamoja na vifaa vinginevyo.