HabariHabari za Kitaifa

Raila kuombolezwa kwa siku saba, kupatiwa mazishi ya kitaifa, atangaza Rais Ruto

Na NDUBI MOTURI Na BENSON MATHEKA October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ametangaza siku saba za maombolezi ya kitaifa kuomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu na kiongozi mkongwe wa upinzani, Raila Amolo Odinga, aliyefariki Jumatano, Oktoba 15, 2025 nchini India alipokuwa akipokea matibabu.

Akihutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi akiwa ameandamana na kaka wa marehemu, Seneta wa Siaya Oburu Oginga, Naibu Rais Kithure Kindiki, pamoja na viongozi wengine wakuu wa serikali, Rais Ruto alisema kuwa taifa litampa Raila mazishi ya kitaifa yenye heshima kamili za kijeshi.

“Ni kwa huzuni kuu na majonzi makubwa ninaarifu Kenya, Afrika na ulimwengu mzima kuhusu kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga,” Rais Ruto alisema katika hotuba ya moja kwa moja.

“Kenya, Afrika na dunia imepoteza nguzo ya demokrasia, shujaa wa uhuru na mtetezi asiyekoma wa utawala bora.”

Katika tangazo hilo, Rais aliamuru kuwa bendera ya taifa ipeperushwe nusu mlingoti katika majengo yote ya serikali, kambi za kijeshi na ofisi za ubalozi za Kenya duniani kuanzia Jumatano hadi jioni ya siku ya mazishi.

Soma pia: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/ndoto-ya-raila-ilivyokosa-kutimia-urais-ukimponyoka-mara-tano/

Viongozi wa juu serikalini, akiwemo Rais, Naibu Rais na mawaziri wote, pia wameamriwa wasitumie bendera ya taifa kwenye magari yao rasmi wakati wa kipindi cha maombolezo.

“Kwa heshima ya Raila Odinga, nimesitisha shughuli zangu zote za umma kwa siku zijazo ili niungane na taifa katika kipindi hiki cha huzuni na tafakari,” Rais alisema.

Rais Ruto pia alitangaza kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi, itakayoongozwa kwa pamoja na Naibu Rais Kindiki na Seneta Oburu Oginga. Kamati hiyo itaratibu shughuli zote za mazishi ya kitaifa.

Serikali, pia, imetuma ujumbe rasmi kwenda India kusimamia usafirishaji wa mwili wa marehemu kurudi nyumbani. Ujumbe huo unaongozwa na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, na unajumuisha Mama Ida Odinga, pamoja na mawaziri Kipchumba Murkomen (Usalama wa Ndani) na Hassan Joho (Madini).

Viongozi wengine kwenye ujumbe huo ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah, Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed, pamoja na wawakilishi wa familia – Jaoko Oburu Odinga na Kevin Opiyo Oginga.

Katika hotuba yake, Rais Ruto alimtaja Raila kama “kiongozi wa aina yake, shujaa aliyeamini katika siasa zenye misingi ya maadili.”

Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/raila-odinga-amefariki-dunia-akiwa-india/

“Jina la Raila Amolo Odinga litaandikwa kwa herufi kubwa katika historia ya Jamhuri yetu – historia ya mapambano, kujitolea, ujasiri, utawala wa sheria na matumaini,” alisema Rais.

Rais alitakia familia ya marehemu – Mama Ida Odinga, watoto wao Rosemary, Raila Jr., na Winnie, pamoja na familia pana ya Odinga na wanachama wa chama cha ODM – pole na faraja kwa kipindi hiki kigumu.

Aliwataka Wakenya wote waungane ili kumuenzi Raila kwa vitendo. “Ndugu Wazalendo, tumepoteza taa ya ujasiri, mnara wa maadili, na baba wa demokrasia yetu,” Rais Ruto alisema.

“Tuungane, kama vile alivyotuhimiza kila mara, si kama wapinzani, bali kama ndugu na dada tunaoshiriki hatima moja.”