Habari

Raila: Tuwape wataalam wa ODM walio serikalini muda wa kuimarisha uchumi

Na ANTHONY KITIMO May 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga ametaka Wakenya wawapatie wataalam wake wa ODM walio serikali muda wa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini.

Bw Odinga anasema kwamba bajeti ya kwanza ya Waziri wa Fedha John Mbadi itakuwa tayari mwezi ujao na itakuwa imetilia maanani matamanio yote ya Wakenya.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba ODM haiko ndani ya serikali.

Raila, wakati huo huo, ametaka serikali kupunguza ushuru kwa raia wanaoteseka na kwamba iangalie mianya yote ambayo pesa za mlipa ushuru zinapotea na kuiziba.

Aidha, amesisitiza kwamba hazina ya maendeleo mashinani (NG-CDF) na Fedha za Barabara zielekezwe kwenye serikali za kaunti kuzisimamia. Asema sio kwamba anataka magavana wawe na pesa nyingi ila ni hitaji la Katiba.

Bw Odinga, ambaye alikuwa akizungumza katika warsha ya ICPAK Mombasa ametaka magavana wote wafisadi wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.