Rais amtaka Sonko ashirikiane na Badi
Na VALENTINE OBARA
RAIS Uhuru Kenyatta amemtaka Gavana wa Nairobi Mike Sonko ashirikiane na Idara ya Kuhudumia Nairobi (NMS) kuendeleza mbele jiji hilo kuu.
Akizungumza Ijumaa wakati wa kuadhimisha Siku ya Mazingira Ulimwenguni, Rais Kenyatta alisema ushirikiano wa Bw Sonko na idara hiyo inayosimamiwa na Meja Jenerali Mohammed Badi utasaidia kuleta mafanikio ya haraka kwa mikakati inayoendelezwa kuboresha kaunti hiyo na viunga vyake.
Wito huo ulitolewa wakati ambapo NMS inaendelea kuonekana ikishikilia shughuli tele za kuendesha jiji, huku makao makuu ya kaunti yakibaki mahame.Katika makubaliano ya Bw Sonko na Ikulu, Kaunti ya Nairobi ilisalimisha idara za Afya, Uchukuzi, Mipango ya Jiji na Ujenzi.
Jukumu lingine lilitajwa kama ‘shughuli nyinginezo za kufanikisha utendakazi’ ambalo wadadisi wanaamini ndilo lilisababisha pia jukumu muhimu la kukusanya kodi za kaunti (idara ya fedha) na usafishaji wa jiji ambao uko chini ya idara ya mazingira, zitwaliwe na serikali kuu.
Wiki iliyopita, Rais Kenyatta alitoa amri ambayo iliifanya NMS kuwa chini ya Afisi ya Rais na hivyo basi kuweka utekelezaji wa mipango yote ya NMS chini yake.Katika amri hiyo, ilibainika kwamba miongoni mwa majukumu makubwa ambayo NMS itatarajiwa kufanikisha ni ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa umma, uboreshaji makao katika mitaa ya mabanda na uboreshaji wa uchukuzi jijini.
Mnamo Ijumaa, Mamlaka ya Kusimamia Mazingira Kitaifa (NEMA) ilichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali mpango wa ujenzi wa nyumba 1,562 katika mtaa wa Pangani, Nairobi.
Wakati huo huo, NMS inaendeleza ukarabati wa barabara za katikati ya jiji ikiwemo kubadilisha maeneo kadhaa ya uegeshaji magari yawe yakitumiwa na waendeshaji baiskeli na wapitanjia.
Ijapokuwa awali Sonko alilalamika sana kwamba alipotia sahihi kwenye makubaliano ya kuikabidhi serikali kuu baadhi ya majukumu, hakujua ilimaanisha NMS ingetwaa majukumu mengi, ameonekana kulegeza msimamo katika siku chache zilizopita.
Wiki iliyopita, alipitisha bajeti ya ziada ya kaunti ambapo, hatimaye, serikali ya kaunti ilikabidhi NMS Sh3.5 bilioni kwa jumla.Hata hivyo aliendelea kusisitiza ni sharti sheria zifuatwe kikamilifu katika utekelezaji wa maelewano kati yake na Serikali Kuu kuhusu ugavi wa mamlaka ya kaunti.
‘Nimeamua kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya wakazi wa Nairobi badala ya siasa duni ambazo zimekumba Nairobi kwa miezi mitatu iliyopita. Kuanzia sasa ninatoa wito kwa kila mmoja wetu tuweke siasa kando, na tutilie maanani hitaji la kuhudumia Nairobi,’ akasema.
Kama njia ya kutaka kudhihirisha utawala wake ulileta mafanikio jijini kwa miaka miwili iliyopita, gavana huyo amekuwa akisambaza picha na video za kuonyesha maendeleo aliyosimamia.
Mnamo Ijumaa, alieleza kuwa ni utawala wake ulioanzisha ukarabati wa barabara ili kuwe na sehemu bora za uendeshaji baiskeli na za wapitanjia.