Habari

Rais awashauri wazazi kuhusu mfumo mpya wa elimu

August 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Ijumaa aliwaambia wazazi kuacha kuwashinikiza watoto wao kujipatia shahada za digrii na kuzingatia mitihani tu na badala yake wasisitize ukuzaji wa talanta za wana wao chini ya mfumo mpya wa elimu unaosisitiza vipawa na ustadi.

Alisema mtaala huo mpya unawapa watoto wa Kenya matumaini na fursa ya kuimarisha vipawa na uwezo wao.

“Tunashinikiza na kukaza watoto kupita mitihani na kujipatia shahada za digrii za vyuo vikuu. Watoto wetu hawana nafasi ya kukua kama watoto,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa Taifa alizungumza katika Jumba la Mikutano la Kenyatta (KICC) alipoongoza ufunguzi rasmi wa Kongamano la Tatu la Kitaifa kuhusu Mageuzi ya Mfumo wa Elimu.

Alisema kila mtoto ana kipawa na jukumu la wazazi ni kukuza talanta hizo.

“Na tufanye kazi pamoja kukuza ujuzi na kustawisha vipawa vya watoto wetu,” Rais aliwaambia wazazi huku akiwaonya dhidi ya kuwalazimisha watoto kusomea taaluma fulani kama vile udaktari “hata pale ni wazi kuwa mtoto anaogopa kuona damu ya mbuzi”.

Rais Kenyatta alisema wazazi mara nyingi hukosa kutambua uwezo wa wanafunzi hata kama watoto wao wangeweza kuwa wanamuziki na wasanii mashuhuri.

“Tunafaa kutayarisha watoto wetu kuwa magwiji wa teknolojia ya mawasiliano kama Bill Gates na marehemu Steve Jobs wa siku zijazo,” akasema Rais akitoa mfano wa Wamarekani hao wawili waanzilishi wa kampuni kubwa za teknolojia za Microsoft na Apple mtawalia.

Kuchochea mabadiliko

Kiongozi wa Taifa alidokeza kwamba utekelezaji kamili wa mfumo huo mpya utachochea mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu na kulinda maslahi ya wanafunzi wote licha ya uwezo wao.

“Wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum watapewa fursa ya kuimarika katika nyanja zao za uwezo na maslahi,” akaeleza Rais Kenyatta akiongeza kuwa mabadiliko ya mtaala yamejikita katika mchakato unaotegemea thamani.

Rais Kenyatta alisema Kenya haina lingine ila kujiwianisha na ukuaji wa haraka kote ulimwenguni na mabadiliko makubwa ya teknolojia kwa kuhakikisha wafanyikazi wake wanapata maarifa ya kisasa humu nchini na kimataifa.

“Mabadiliko hayo ni muhimu iwapo tunataka kuwa na elimu bora ambayo inawafanikisha wanafunzi kushindana vizuri kwenye sekta ya wafanyikazi ulimwenguni,” akasema.

Akigusia mafanikio ya utekelezaji wa mfumo mpya unaojikita kwa uamilifu (CBC), Rais Kenyatta alisema Serikali iko tayari kutekeleza awamu ya Gredi 4 mwaka ujao 2020 na akapongeza tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) kwa kuwafunza walimu 113,223 kutoka shule za umma na za kibinafsi kuhusu CBC.

Alitoa changamoto kwa Wizara ya Elimu na Tume ya Kuwaajiri Waalimu nchini TSC kudumisha kasi hiyo akisema “walimu wanastahili kuwa mashujaa wetu wakuu kubadilisha mtaala wetu”.

Kabla ya kongamano hilo Wizara ya Elimu iliandaa mikutano mbalimbali ya mashauriano kuhusu ubora wa elimu katika Kaunti zote 47 mbali

Kwa ujumla iliandaa makongamano 11 ya sekta mbali mbali mbeleni ambayo yalitoa nafasi kadhaa kwa washika dau kutoa kauli zao kuhusu mtaala huu unaohimiza umilisi na utendaji.

Msomi maarufu wa Ghana na Naibu Waziri wa Elimu ya Msingi na Sekondari Dkt. Yaw. O Adutwum alikuwa mzungumzaji mkuu kwenye kongamano hilo

Wengine waliohutubu ni Waziri wa Elimu Profesa George Magoha na Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia miongoni mwa wengine.