Rais azinduka baada ya umaarufu wake kupungua
MWANGI MUIRURI na LEONARD ONYANGO
ZIARA mbili alizofanya Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumapili na Jumatatu katika Kituo cha Kontena (ICD) cha Embakasi zilitokana na ripoti za kushuka kwa umaarufu wake eneo la Kati.
Duru ziliambia Taifa Leo kuwa ripoti kuhusu malalamiko ya wafanyibiashara wa masoko ya Kamukunji, Nyamakima na Gikomba jijini Nairobi zilimzindua ndiposa akaamua kuzuru ICD kujionea hali halisi.
Kwenye ziara hizo, Rais Kenyatta aliagiza kontena zote ambazo zimerundikana Embakasi ziondolewe katika muda wa wiki tatu, na akaonya wale ambao wanataka kukwepa kuzilipia ushuru kuwa watachukuliwa hatua kali.
Rais alitangaza kuwa Serikali itasajili waagizaji aina tofauti za mizigo kwenye kontena moja ili kuondoa na wanaokwepa ushuru.
Alisema ni watakaosajiliwa pekee ambao watakubaliwa kuingiza mizigo kwa niaba ya wafanyibiashara wadogo.
Kulingana na duru, ziara hizo zilikuwa za kwanza kwenye msururu wa zingine ambazo zimepangwa za Rais kuzuru mashinani na kutangamana na wananchi katika juhudi za kubadilisha maoni ya wengi kuhusu serikali.
Rais alifanya ziara hizo huku wabunge kadhaa wa eneo la Mlima Kenya wakimtaka awafute kazi mawaziri 16 kwa kile wanachosema ni kushindwa kufanya kazi yao.
Mbunge wa Kieni, Kanini Kega alisema jana kuwa idadi kubwa ya mawaziri wamelemewa na kazi na wanafaa kuondolewa ili kutoa nafasi ya kuteuliwa kwa walio na uwezo wa kusimamia wizara zao kikamilifu.
Bw Kanini alisema wengi wa mawaziri wanajishughulisha na mambo yao ya kibinafsi huku wengine wakitumia vyeo vyao kujiandaa kuwania nyadhifa za kisiasa 2022.
“Namwomba Rais Kenyatta avunje Baraza la mawaziri kwa sababu wameshindwa kazi. Ni sita hivi ambao wanaonekana kufanya kazi. Ikiwa bajeti ijayo itatekelezwa na mawaziri waliopo sasa, nasikitika hali ya nchi itaendelea kuwa mbaya,” akasema.
Alieleza kuwa mawaziri wengi walioko sasa hawazingatii masuala ya kitaifa mbali ya maeneo yao: “Kwenye mapendekezo ya bajeti ijayo, ilikuwa wazi karibu wote waliweka miradi katika maeneo wanakotoka kwa nia ya kujiuza wakilenga kuchaguliwa 2022,” akaeleza.
Mbunge huyo alisema matatizo ambayo yanakumba sekta mbalimbali za kiuchumi yametokana na mawaziri kutotilia maanani kazi zao na matokeo yake kwa wananchi, na pia kutoa ushauri usiofaa kwa Rais.
Mbunge huyo alisema itakuwa vigumu kuafikia Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kwa wakati uliosalia kabla ya 2022, lakini akaeleza kuna matumaini ya kaunti za Kitui na Makueni kufanikiwa.
Maoni ya sawa na hayo yemetolewa na mbunge wa Mathira Rigathi?Gachagua na Moses Kuria wa Gatundu Kusini.