Habari

Rais Kenyatta aagiza wadau muhimu wahakikishe wanafunzi wote wanarejea shuleni Januari

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

YAMEBAKI majuma machache tu shule zote na taasisi za elimu ya juu nchini zifunguliwe tena na kwenye hotuba yake kwa taifa, Rais Uhuru Kenyatta amewataka wazazi na wadau wengine muhimu kuhakikisha watoto na wanafunzi wengine wanarejea shuleni kuanzia Januari 4, 2021.

Waziri wa Usalama wa Ndani ni Fred Matiang’i naye Waziri wa Elimu ni Prof George Magoha.

“Ili kuhakikisha hili linatimia, ninaamuri Wizara ya Usalama wa Ndani kupitia machifu na manaibu wao kuhakikisha watoto wa maeneo yao wanafungua,” Rais Kenyatta ameagiza.

Licha ya wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kurejea shuleni Oktoba 2020 ili kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa, baadhi ya shule zimeripoti watoto na walimu kuambukizwa virusi vya corona.

Jamhuri Dei ya mwaka huu imekuwa tofauti, hasa kutokana na upungufu wa watu waliohudhuria maadhimisho hayo katika uwanja wa michezo wa Nyayo, jijini Nairobi, kufuatia sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia maenezi ya virusi vya corona.

Naye Naibu Rais William Ruto amesema umoja wa taifa na ushirikiano utasaidia kulikabili janga la Covid-19.

Akisikitikia athari za virusi vya corona katika ukuaji wa taifa, utangamano wa watu na pia kwenye ulingo wa siasa, Dkt Ruto amesema umoja wa wananchi, hasa kutii sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kupambana na ugonjwa huu ambao ni janga la kimataifa, utanusuru taifa.

“Baada ya majuma matatu kuanzia sasa, karibu watoto wetu milioni 14 watarudi shuleni, mwaka mmoja baada ya shule kufungwa kutokana na janga la corona.

“Tunahitaji umoja kama taifa. Ninaamini kama akina baba zetu walivyopigania uhuru wa Kenya, tutashinda changamoto zinazotukumba,” amesema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais amesema hayo leo Jumamosi, Desemba 12 katika maadhimisho ya Jamhuri Dei 2020.

Kinyume na tamasha zingine za kitaifa, kabla ya Covid-19, viongozi kadha wa serikali na pia wanasiasa waliokuwa wakipewa jukwaa kuzungumza, Jamhuri Dei 2020 Naibu Rais Ruto na Rais Kenyatta na ambaye ameongoza maadhimisho hayo, ndio pekee wametoa hotuba kwa taifa.