Habari

Rais Kenyatta, Raila kukabidhiwa ripoti ya BBI Jumanne

November 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WALTER MENYA

WANACHAMA wa Jopo la Maridhiano (BBI) watakutana na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga Jumanne, Novemba 26 kuwakabidhi ripoti.

Hayo yamesemwa Ijumaa na mwenyekiti wa BBI Yusuf Haji aliyehutubia wanahabari Ijumaa jijini Nairobi.

“Ni fahari yetu kujulisha umma kwamba mkutano wa kuwapokeza ripoti viongozi wetu umeratibiwa Jumanne, Novemba 26, 2019,” amesema Bw Haji.

Jopokazi hilo lilikamilisha shughuli zake Oktoba 23, 2019.

Novemba 15, 2019, Rais Kenyatta alikutana na viongozi wa kutoka eneo la Mlima Kenya ambapo alitoa hadi kwamba ripoti hiyo itatoleshwa nakala nyingi na kusambazwa kwa umma ili Wakenya waelewe yaliyomo.

BBI ilichapishwa rasmi katika gazeti la serikali Mei 24, 2018, ikiwa ni muda wa miezi michache tu tangu zishuhudiwe salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Bw Odinga mnamo Machi 2018.

Zilimaliza au kwa kiwango kikubwa kupunguza uhasama ulioshuhudiwatangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Katika chama cha Jubilee, salamu za maridhiano zilichangia pakubwa kuchipuka kwa makundi mawili makuu; ‘Kieleweke’ wanaomuunga mkono Rais Kenyatta na ‘Tangatanga’ wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto.