Rais Mstaafu Daniel Arap Moi azikwa nyumbani Kabarak
Na SAMMY WAWERU
MIAKA 42 iliyopita, taifa lilimpoteza Rais Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kenya ndiye Mzee Jomo Kenyatta.
Rais huyo wa kwanza, aliaga dunia Agosti 22, 1978, akiwa madarakani na waliokuwa wamezaliwa wakati huo walishuhudia heshima alizopata Hayati Mzee Kenyatta akizikwa, katika hafla ya kitaifa na iliyoongozwa na kikosi cha kijeshi.
Rais aliye mamlakani ndiye Amiri Jeshi Mkuu, hivyo basi amri zote katika kikosi hicho ziko chini yake.
Kwa mujibu wa mila, itikadi na desturi za wanajeshi, mmoja wao anapofariki akiwa kazini, yaani kabla kustaafu, anazikwa katika hafla ya kipekee ambapo mizinga 21 hufyatuliwa hewani, kuonyesha heshima kwa mwendazake.
Rais akiwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu, akifariki akiwa mamlakani anazikwa katika hafla ya kitaifa ambayo inaongozwa na wanajeshi wenye madaraka ya hadi ya juu katika kikosi cha KDF.
Wakati wa kuteremsha jeneza lake kaburini, mizinga 21 inafyatuliwa.
Kwa muda wa wiki moja iliyopita, kifo cha aliyekuwa Rais wa pili wa Kenya, Mzee Daniel Toroitich Arap Moi, kimefichua mengi kuhusu mila, itikadi na tamaduni za kikosi cha kijeshi. Pia, kimekumbusha walioshuhudia kifo cha Mzee Jomo Kenyatta, heshima alizopokezwa wakati akizikwa.
Mzee Moi alifariki mnamo Jumanne, Februari 4, 2020, Nairobi Hospital na Rais Uhuru Kenyatta ndiye alitangaza rasmi kifo cha Rais huyo mstaafu.
Kilichofuata, kikawa mwili wa mwendazake kusafirishwa na wanajeshi kutoka wadi ya kipekee aliyokuwa akihudumiwa ili kuhifadhiwa katika Hifadhi ya Maiti ya Lee jijini Nairobi.
Ulinzi uliimarishwa vikali katika hifadhi hiyo, wanajeshi waliovamilia sare rasmi, nyekundu, wakisimama kwenye lango usiku na mchana. Walioruhusiwa kuutazama mwili wa Mzee Moi ni watu wa familia, marafiki wa karibu na viongozi wakuu serikalini.
Wizara ya Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali, chini ya Waziri Dkt Fred Matiang’i na Katibu wake Dkt Karanja Kibicho, ilichukua hatamu ya maandalizi ya mazishi, ikiwa ni pamoja na mikakati ya kumuomboleza Moi.
Baada ya kutangaza kifo cha Rais huyo Mstaafu, kiongozi wa taifa Uhuru Kenyatta, pia alisema Mzee Moi ataombolezwa hadi atakapozikwa, ikiwa ni Jumatano, Februari 12, 2020. Mzee Jomo Kenyatta, ambaye ni babake Rais Kenyatta, aliombolezwa kwa muda wa siku 30.
Wakenya walipata fursa ya kuutazama mwili wa Mzee Moi, katika majengo ya bunge jijini Nairobi, ambapo shughuli hiyo ilichukua siku tatu.
Kulingana na bunge ni kwamba zaidi ya watu 200,000 waliutazama mwili wa marehemu.
“Kufikia Jumatatu jioni, zaidi ya watu laki mbili walikuwa wameutazama mwili wa Rais Mstaafu Mzee Daniel Toroitich Arap Moi,” Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi alisema baada ya wabunge kushiriki kikao cha kutuma salamu zao za pole.
Majengo ya bunge na mazingira yake, usalama uliimarishwa, vikosi vya pamoja kutoka idara ya jeshi na polisi wakishika doria katika kila kona.
Mwili wa Mzee Moi ulikuwa ukisafirishwa kwa gari maalum la kijeshi, kutoka Hifadhi ya Lee Funeral hadi majengo ya bunge na pia kurejeshwa, chini ya ulinzi mkali.
Mapema Jumatano, mwili wa Mzee Moi ulisafirishwa kwa ndege ya kijeshi, seneta wa Baringo na ambaye pia ni mwanawe aliandamana nao hadi nyumbani Kabarak, Kaunti ya Nakuru kwa ibada ya mazishi.
Rais Kenyatta ameongoza Wakenya katika kumpungia mkono wa buriani.
Aidha, Mzee Moi amezikwa chini ya itakadi za kijeshi, na kwa kuwa aliwahi kuhudumu kama Amiri Jeshi Mkuu mizinga 19 imefyatuliwa. Ndege za kivita, pia zimepita angani, yote hayo yakiashiria heshima kwa Rais huyo Mstaafu.
Mzee Moi alitawala Kenya kati ya 1978 – 2002.
Viongozi mbalimbali wamemmiminia sifa kemkem, wakimtaja kama kiongozi mzalendo aliyependa nchi yake, amani na umoja na zaidi ya yote Mcha Mungu.
Buriani Mzee Daniel Toroitich Arap Moi.