HabariSiasa

Rais nisamehe, watu wananidharau sasa, Echesa alia

May 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

ALIYEKUWA Waziri wa Michezo Rashid Echesa sasa anamlilia Rais Uhuru Kenyatta kumsamehe na kumwokoa kutokana na masaibu ambayo yamekuwa yakimwandama tangu atimuliwe serikalini.

Kulingana na Bw Echesa, Rais Kenyatta anafahamu masaibu yake ya hivi karibuni ambapo alikamatwa kwa madai ya kufadhili magenge ya wahalifu, akidai sasa watu wanamdharau.

“Mtu wa hadhi yangu kukamatwa ni lazima kuwe na mashauriano kati ya Rais na Wizara ya Usalama. Ninaamini kuwa kulikuwa na ushirikiano.

“Rais ana nambari yangu ya simu na mawaziri wenzangu pia wana nambari yangu ya simu. Ikiwa wanahisi kuwa kuna kitu wanachofaa kujua kuhusu mimi, wangenipigia simu kuliko kuniaibisha kiwango hicho bila kufanya uchunguzi,” akasema Echesa.

Waziri huyo amejutia kuunga mkono Rais Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 2017 huku akisema kuwa hatua hiyo ilimfanya kubwagwa katika kinyang’anyiro cha ubunge.

“Uhuru Kenyatta ni sawa na baba yangu ni namjua rais kama mtu muungwana. Hiyo ndiyo maana katika uchaguzi wa 2017 niliwania nikapoteza kiti cha ubunge kutokana na msimamo wangu wa kusimama na Uhuru.

“Ikiwa ningewania kwa kutumia chama maarufu tofauti na Jubilee leo ningekuwa mbunge,” akasema Bw Echesa.

Waziri huyo wa zamani alisisitiza kuwa kufikia sasa hajui kilichomfanya Rais Kenyatta kumtimua kutoka wadhifa wake wa uwaziri.

“Hajawahi kunieleza kwa nini alinitimua. Sasa rais ananiabisha. Ni jukumu la rais kupanga na kupangua serikali yake anavyotaka. Niliuliza kwa nini nilitimuliwa sikuambiwa na nikaendelea na maisha yangu ya kawaida,” akasema Bw Echesa.

“Ninachotaka kueleza rais ni kwamba ikiwa kuna kitu nilikukosea kilichokuudhi na hutaki kunieleza, tafadhali rais nisamehe,” akaongezea.

Bw Echesa alionekana kuashiria kwamba alikuwa tayari kuacha kumpigia debe Naibu wa Rais William Ruto endapo hatua hiyo ingemsababisha kujipata pabaya.

“Ikiwa kuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto ndilo kosa inafaa niambiwe. Nakumbuka tulipokuwa tukimpigia kampeni katika uchaguzi uliopita alitueleza kuwa mnisaidie na nikimaliza muhula wangu tutakampigia debe Dkt Ruto.

Hivyo ndivyo tunafanya sasa, ikiwa hilo ndilo kosa basi ninafaa kuambiwa. Kuunga mkono naibu wa rais si jambo la kufa kupona,” akasema.