Habari

Rais Ruto atanunua mashine ya kutengeneza chapati milioni moja kwa siku

Na FRIDAH OKACHI March 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ameahidi kumnunulia Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, mashine ya kutengeneza chapati inayoweza kupika milioni moja kwa siku ili kuimarisha mpango wa lishe wa shule wa ‘Dishi Na County’ jijini Nairobi.

Alikuwa akizungumza katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St Teresa, eneo la Mathare jijini Nairobi, Jumanne, Machi 11, 2025 ambapo wanafunzi walimwomba gavana aongeze chapati kwenye orodha ya chakula cha mpango huo.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja aliomba Rais Ruto amsaidie kupata mashine hiyo ambayo itanufaisha wanafunzi 300,000.

“Mpango huu; hiyo inamaanisha tunahitaji mashine ya kuzalisha chapati milioni moja kila siku. Nimeomba Rais atusaidie kupata mashine hiyo,” alisema gavana huyo.

Rais Ruto alikubali ombi hilo na kuwaambia wanafunzi, atawezesha mpango huo.

“Nimekubali kununua mashine ya kutengeneza chapati. Gavana, kazi yako sasa ni kutafuta mahali pa kuinunua,” alisema Rais Ruto.