RASMI: Kwaheri noti nzee ya 'thao'
Na VALENTINE OBARA
NOTI nzee ya Sh1,000 hatimaye imegeuka karatasi isiyo na thamani yoyote, baada ya muda wa mwisho wa matumizi yake kukamilika Jumatatu jioni.
Noti hiyo imeingia kwenye orodha ya sarafu nyingine zisizo na maana katika soko la fedha nchini kama vile peni, ndururu na nyinginezo.
Benki Kuu ya Kenya (CBK) sasa inatarajia kufanya tathmini ya kubainisha idadi kamili ya noti hizo zilizokusanywa katika mabenki na kufahamu kama kuna kiwango chochote ambacho kingali mikononi mwa watu.
Noti zote zilizokusanywa, ambazo zinatarajiwa kufika mabilioni ya pesa zitaharibiwa, kwa mujibu wa CBK.
Noti hiyo ilianza kutumiwa katika mwaka wa 1994 na ikawa ndiyo sarafu kubwa zaidi ya Kenya.
Katika miaka hiyo yote 25, noti ya Sh1,000 ambayo sasa imeondolewa katika soko la kifedha ilibandikwa majina si haba, mengi yakiashiria sifa za ukuu wake.
Miongoni mwa majina ya utani ambayo noti hiyo ilipata katika maeneo tofauti ya nchi ni kama vile ngiri, tenga, ndovu na thao. Mitaani, watu ambao ni weupe waliishia kusemekana kuwa wenye ‘rangi ya thao’.
Sifa zake hazikukosekana pia katika miziki ya humu nchini, kupitia kwa picha za wasanii waliotaka kuonyeha maisha ya kifahari katika video zao, au kutajwa kama sehemu ya nyimbo.
Mojawapo ya tungo maarufu ambapo noti hii ilitajwa ni katika wimbo wa msanii wa kufoka Juliani unaofahamika kama ‘biceps’ kwamba: “Wanabeba mandovu kwa wallet…lakini hawana nguvu ya kutoa msumari imewafunikia kwa casket.”
Mstari huo ulilenga kuonyesha kwamba licha ya utajiri ambao mtu anao (kubeba ‘ndovu’ kwa pochi), hakuna atakayefanikiwa kuepuka kifo na hivyo basi binadamu wote ni sawa kiuhai.
Noti mpya ya Sh1,000 ambayo ilizinduliwa Juni 1 wakati wa sherehe za Madaraka Dei pia ina picha ya ndovu kando na ile ya Bunge la taifa.
Ingawa CBK ilizindua pia noti mpya za Sh50, Sh100, Sh200 na Sh500, Gavana wa benki hiyo Patrick Njoroge alisema nia ya kuanza kwa kuondoa Sh1,000 ni kwa vile imekuwa ikitumiwa sana kwa njama za ufisadi.
Ijapokuwa Kenya imewahi kuondoa sarafu nyingine katika soko la kifedha miaka iliyopita, hii ilikuwa mara ya kwanza kuondoa sarafu kubwa zaidi kwa kipindi kifupi cha miezi minne pekee.
Mnamo Juni wakati shughuli hiyo ilipoanzishwa, kulikuwa na noti 217.6 milioni za Sh1,000 zilizokuwa zikitumiwa. Hii ni sawa na Sh217.6 bilioni.
Kufikia wiki iliyopita, haikufahamika wazi kiwango kamili cha hela hizo zilikuwa zimerudishwa ijapokuwa Dkt Njoroge alisema ni watu 24 pekee walirudisha zaidi ya Sh2 milioni kila mmoja.
Hii iliashiria kwamba, huenda wengine waliokuwa wameshikilia kiwango kikubwa cha noti hizo walizirudisha kwa kiasi kidogo kidogo kuepuka kuulizwa maswali mengi katika benki, au pengine waliamua kuzibadilisha ziwe sarafu za kigeni.
CBK haikuwa imetoa taarifa zaidi kuhusu kiwango kilichokusanywa kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa