REFERENDA: Wabunge kuamua kuhusu terehe ya uchaguzi
HUENDA Wakenya wakashiriki kura ya maamuzi ikiwa wabunge Jumatano wataupitisha mswada unaolenga kubadilishwa tarehe ya uchaguzi mkuu kutoka Agosti hadi Desemba.
Hii ni kwa sababu mswada huo wa marekebisho ya Katiba utaongeza muda wa kuhudumu kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa miezi minne zaidi ikiwa uchaguzi mkuu utafanyika Desemba 2022.
Kuongeza kuwa muda wa kuhudumu kwa Rais ni mojawapo ya masuala ambayo sharti yabadilishwe kupitia kura ya maamuzi, kulingana na kipengee cha 255 cha katiba ya sasa.
Mswada huo ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa (pichani) unapendekeza tarehe ya uchaguzi ibadilishwe kutoka Jumanne ya pili mwezi Agosti kila baada ya miaka mitano baada ya uchaguzi mkuu hadi Jumatatu ya tatu mwezi Desemba miaka mitano baada ya uchaguzi.
Mnamo Alhamisi, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alisema Rais ndiye ataamua ikiwa mswada huo utawasilishwa kwa raia kwa kura ya maamuzi endapo utaungwa mkono na angalau wabunge 233 katika kura itakayopigwa bunge leo alasiri.
Hii ni baada ya mswada huo kuwasilishwa katika bunge la Seneti na kupitishwa na angalau maseneta thuluthi mbili yao, yaani maseneta 45 kati ya maseneta wote 67.
‘Ningependa kuwajulisha wabunge kwamba uamuzi kuhusu mswada huo wa marekebisho ya katiba ili kubadili tarehe ya uchaguzi mkuu utafanywa Jumatano alasiri,’ akasema Bw Muturi.
‘Iwapo wabunge 233 watapiga kura kuunga mkono mswada huo baada ya kujadiliwa kwa Hatua ya Pili (Second Reading), Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC) itauorodhesha ili ujadiliwe kwa Kamati ya Bunge lote ambayo itafanyika katika vikao vijavyo. Baadaye mswada huu utawasilishwa kwa seneti,’ akawaambia wabunge.
Bw Muturi alisema wajibu wa Bunge ni kutekeleza mamlaka yake katika uundaji wa sheria kwa kupitisha mswada wa kuifanyia Katiba marekebisho.
‘Baada ya mswada huu kupitishwa katika mabunge yote mawili na kuwasilishwa kwa rais ili autie saini, itakuwa ni wajibu wa Afisi ya Rais kuamua kama mswada huo unahusu masuala ambayo yameorodheshwa katika kipengee cha 255.
Masuala katika kipengee hicho ni yale ambayo sharti yaamuliwe kupitia kura ya maamuzi, kama vile kuongezwa kwa kipindi cha kuhudumu kwa rais na kubadilishwa kwa mfumo wa uongozi, kati ya mengine.
Mengine ni yale yanahusu; Ukuu wa Katiba, Mipaka ya Kenya, Mamlaka ya wananchi, Maadili ya kitaifa na kanuni za uongozi, Sura kuhusu Haki, Idara ya Mahakama, Bunge, Serikali ya Ugatuzi na Tume za Kikatiba.
Spika Muturi alisema hoja ya kupigia kura mswada huo ikifeli kuuungwa mkono na angalau wabunge 233, anaweza kutoa nafasi nyingine kwa bunge kuamua kuhusu suala hilo, kulingana na mamlaka aliyepewa katika sheria ya bunge nambari 62 (2).