Habari

Ripoti: Walipa ushuru wamekamuliwa Sh4.5 bilioni kupeleka polisi Haiti

Na DAVID MWERE March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JUHUDI za kuleta amani nchini Haiti zimewagharimu walipa ushuru Sh4.5 bilioni ndani ya miezi tisa iliyopita wakati ambapo serikali inakabiliwa na uhaba wa fedha za kugharamia mahitaji ya sekta muhimu kama afya na elimu.

Maafisa 800 wa polisi wa Kenya wako katika taifa hilo la eneo la Caribbean kupambana na magenge ya wahalifu yaliyoteka sehemu kubwa ya jiji kuu Port-au-Prince.

Polisi wa Kenya wanaongoza kikosi cha walinda usalama kutoka mataifa mbali walioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), japo halifadhiliwi na Umoja wa Mataifa (UN).

Hii ina maana kuwa shughuli za walinda usalama hao wa kigeni (MSSM) zinafadhiliwa kwa michango kutoka kwa mataifa wanachama ikiwemo Amerika iliyokatiza mchango wa Sh1.7 bilioni baada Rais Donald Trump kuingia mamlakani mwaka huu.

Mnamo Jumatano, Bunge la Kitaifa lilipitisha Sh7.5 bilioni zaidi kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), pesa zinazojumuisha Sh2.5 bilioni kufadhili “shughuli za kuleta amani Haiti.”

Mgao wa Fedha hizo uko katika Bajeti ya Ziada ya Pili ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 iliyopitishwa na Bunge.

Mgao wa fedha kwa shughuli za Haiti unaongezea Sh2.1 bilioni zilizotengwa katika Bajeti ya Ziada ya Kwanza iliyopitishwa Desemba mwaka jana.

Mnamo Juni 24, 2024 kundi la kwanza la maafisa 200 walitumwa Haiti huku wengine 600 wakipelekwa nchini humo Januari mwaka huu.

Pesa zote za kugharamia mahitaji ya polisi wa Kenya walioko Haiti zilipitishwa kwenye bajeti mbili za ziada.

Awali, serikali iliwahakikishia Wakenya kwamba kibarua cha kuleta amani Haiti kingefadhiliwa na UN.

Alhamisi, Katibu wa Wizara ya Fedha Chris Kiptoo na mwenzake wa Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei hawakujibu maswali yetu kuhusu mantiki ya fedha za umma kutumika kwa shughuli za kuleta amani Haiti.

Lakini Desemba mwaka jana, Waziri wa Fedha John Mbadi alitetea hatua ya serikali kutumia fedha za umma kugharamia shughuli hiyo akisema “inaashiria kujitolea kwa Kenya kusaidia ndugu zetu wa Haiti.”

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA