Habari

Ripoti ya BBI iko karibu, mimi na Rais tutaipokea punde – Raila

October 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

PATRICK LANG’AT na JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga alidokeza Jumapili kuwa ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) itatolewa hivi karibuni ili kutoa nafasi kwa maandalizi ya kura ya maamuzi.

Bw Odinga alisema yeye na Rais Uhuru Kenyatta watapokezwa ripoti hiyo, miezi mitatu baada ya jopokazi lililoongozwa na Seneta Yusuf Haji kukamilisha kuitayarisha mnamo Juni 30.

“Ripoti ya BBI sasa iko tayari. Baada ya siku chache tu Uhuru na mimi tutaipokea. Na tutaisambaza ili kila mtu aisome. Kwa hivyo, nashangaa ninaposikia watu wengine wakiipinga. Mbona unapinga kile ambacho haujaona?” Bw Odinga akauliza.

Alikuwa akiongea katika Kanisa la United Christian Ministries, Kawangware, Nairobi.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na Mbunge wa eneo hilo (Dagoretti Kaskazini) Simba Arati na wabunge; Maina Kamanda (Mbunge Maalum), George Aladwa (Makadara), Elisha Odhiambo (Gem), Justus Kizito (Shinyalu) na mbunge wa Ruaraka Tom Kajwang.

Wengine walikuwa Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Mpuru Aburi, Seneta Maalum Gertrude Musuruve na Mbunge Maalum Dennitah Ghati.

Bw Odinga alisema sharti Wakenya wajadiliane kuhusu namna watakavyozalisha mali ya kitaifa ambayo imepungua.

“Sharti mtoto azaliwe. Na mtoto ni Katiba Mpya,” akasema Bw Kajwang.

Bw Kizito akasema, “Tuna shida nchini Kenya, na Raila, Uhuru na Handisheki ndio suluhu.

Kwa upande wake, Bw Kamanda alimwidhinisha Bw Odinga kwa urais wa 2022, akisema taifa hili liko tayari kwa uongozi wake.

“Haturudi nyuma. BBI ndiyo suluhu ambayo Kenya imekuwa ikisubiri. Wakati wa kutekelezwa kwa mageuzi yanayopendekezwa na BBI ni sasa. Ripoti itolewe kisha tuipitishe.”

Wale watakaoipinga wako huru kufanya hivyo lakini wajue kwamba watashindwa. Taifa hili sharti lijiandae kwa BBI na urais wa Raila mnamo 2022,” akasema Bw Kamanda.

Mbunge huyo Maalum alipuuzilia mbali kampeni ambazo Naibu Rais William Ruto anaendesha katika eneo la Mlima Kenya akisema kuwa hazitazaa matunda yoyote.

“Usiwe na wasiwasi wowote kuhusu Mlima Kenya. Tuko sawa. Kile tunahitaji ni Uhuru na Raila kufanya mikutano miwili huko na ushawishi wake utayeyushwa,” akasema Bw Kamanda.

Bw Aladwa alisema ingawa Bw Odinga hajatangaza azma yake ya kuwania urais 2022 “watu wanamtaka kufanya hivyo na wamemwidhinisha.”

“Raila ndiye atakuwa Rais mnamo 2022. Hii ndio maana tunawambia wapinzani wetu kukoma kumtusi Raila na Uhuru,” akasema.

Kabla ya Bw Odinga kuzungumza kuhusu BBI Jumapili, maswali yalikuwa yameibuliwa kuhusu ni kwa nini muda mrefu umepita kabla ya yeye na Rais Kenyatta kupokezwa ripoti hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany alisema wakereketwa wa BBI “wanaogopa kutoa ripoti hiyo kwa umma kwani itakataliwa.”

“Hatuna habari zozote kuhusu BBI. Raila amekuwa akiizungumzia sana, ni yeye anafahamu yaliyomo kwenye ripoti hiyo,” Bw Kositany ambaye ni Mbunge wa Soy akaeleza