Habari

Ripoti yasema majanga kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaongeza matatizo ya akili

Na MWANDISHI WETU January 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RIPOTI ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2024 imeiweka Kenya katika nafasi ya nne barani Afrika kwa idadi ya watu walioathiriwa na matatizo ya afya ya akili, wanaokadiriwa kuwa milioni 1.9 huku wataalamu wakisema mabadiliko ya tabia nchi yanachangia hali hii.

Ripoti hiyo ilitaja mabadiliko ya tabianchi kama sababu kubwa inayochangia matatizo ya afya ya akili. Majanga kama mafuriko, ukame na maporomoko ya ardhi hutokea ghafla bila tahadhari, jambo linafanya waathiriwa kuchukua muda mrefu kupona.

Watu wanaonusurika majanga hayo huweza kukumbwa na viwango vya juu vya wasiwasi, hali ambayo huweza kusababisha mfadhaiko mkubwa.

Kwa mfano, mvua kubwa iliyoshuhudiwa mwaka 2019 na 2020 ilisababisha Mto Kuja kufurika katika Kaunti ya Migori, na kuwalazimu maelfu ya wakazi wa vijiji vitatu kuhama makazi yao huku nyumba, shule na mashamba yakifunikwa na maji. Takriban watu 10 walipoteza maisha.

Dkt Boniface Chitayi, daktari wa magonjwa ya akili katika Wizara ya Afya na Rais wa Chama cha Madaktari wa Akili Kenya, anasema matukio yanayosababisha kupoteza mali, wapendwa na kuhama makazi huongeza viwango vya mfadhaiko na wasiwasi. Aliongeza kuwa kukabiliana na mabadiliko ya ghafla si rahisi.

Upatikanaji wa huduma za afya ya akili bado ni changamoto kwani ni kaunti 22 pekee kati ya 47 zinazotoa huduma hizo, hali inayosababisha uchunguzi usio sahihi. Katika kaunti ya Migori, vijana walio chini ya umri wa miaka 35 wanachangia asilimia 66 ya visa vya afya ya akili vilivyoripotiwa mwaka huu.

Kadri visa vinavyoongezeka, kuna haja ya bajeti mahsusi ya afya ya akili. Licha ya magonjwa ya akili kuchangia asilimia 13 ya mzigo wa magonjwa, yalitengewa asilimia 0.1

Dkt Frank Njenga, Makamu Mwenyekiti wa jopo kazi kuhusu afya ya akili, anasema Wakenya wengi hawatofautishi kati ya afya ya akili na ugonjwa wa akili, huku ukosefu wa uhamasishaji ukiendelea kuwa kikwazo kikubwa. Utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Afya ya Akili 2021–2025 unaweza kutoa mwelekeo thabiti kwa taifa na kaunti.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Akili ya Kenya (2015–2030), mfadhaiko ulibainika kuwa ugonjwa wa akili unaoathiri Wakenya wengi. Aidha, jopo kazi la serikali kuhusu afya ya akili iliyoundwa Desemba 2019 ilifichua kuwa angalau asilimia 25 ya wagonjwa wa kutibiwa na kurudi nyumbani na asilimia 40 ya wagonjwa wa kulazwa hospitalini wamewahi kuathiriwa na ugonjwa wa akili.