Ruku akana madai ya kupanga kuvuruga mikutano ya Gachagua Mbeere
WAZIRI wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, amepuuzilia mbali madai kuwa anapanga njama ya kuwakodi wahuni kusambaratisha mikutano ya kampeni iliyoratibiwa kuongozwa na kiongozi wa chama cha DCP Rigathi Gachagua katika eneobunge la Mbeere Kaskazini.
Bw Ruku alimsuta Bw Gachagua kwa kujaribu kumhusisha na kanda ya video inayosambaa mitandaoni ikiwaonyesha watu fulani wakitisha kuzua fujo.
“Nimeona barua iliyoandikwa na kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua ikirejelea kanda moja ya video inayodai kumwonyesha Bw Simon Njagi Njiru almaarufu Gikundo Wa Gikundo, Bw Josiah Kariuki Ngari na Susan Nyaga miongoni mwa wengine wakitisha kushambulia wakazi wa Mbeere Kaskazini na yeye mwenyewe atakapoenda kumfanyia kampeni mgombeaji wa mrengo wake mnamo Novemba 15.”
“Katika barua hiyo Gachagua anadai kuwa wale wanaotoa vitisho hivyo ni wandani wangu wa karibu. Pia anadai kuwa ninawalazimishia wakazi wa Mbeere Kaskazini kiongozi,” Bw Ruku akasema kwenye taarifa.
Hata hivyo, waziri huyo alikiri kuwa anawafahamu Bw Josiah Kariuki na Susan Nyaga. Lakini akasisitiza kuwa hawezi kuwajibikia shughuli za kibinafsi za watu hao.
“Kwa hivyo, barua ya Gachagua haina msingi wowote na inalenga tu kuibua hisia za umma na chuki dhidi yangu,” Bw Ruku akasema.
Alisema kwamba ikiwa kweli Bw Gachagua amehisi kukerwa na kanda hiyo, anafaa kuwasilisha malalamishi yake kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) au kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja wala si kuandika barua ya kuitoa kwa umma.
“Gachagua alifaa kufika katika afisi yoyote ya DCI katika ngazi za kanda, kaunti au kaunti ndogo na hata kituo cha polisi kurekodi taarifa,” Bw Ruku akasema.
Alieleza kwamba Bw Gachagua anafahamu fika kwamba DCI ina mamlaka kisheria kupokea malalamishi kutoka kwa umma na kuyanakili kabla ya kuanza uchunguzi rasmi.