Ruto aahidi kutatua mzozo wa wabunge na maseneta
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto ameahidi kuingilia kati mvutano kati ya wabunge na maseneta kuhusu kiasi cha fedha ambazo zinapsa kutengewa serikali za ili kuziepusha serikali za kaunti na changamoto za kifedha kuanzia Julai.
Akiongea Jumanne alipoongoza kikao cha Baraza Shirikishi kuhusu Bajeti na Masuala ya Uchumi (Intergovernmental Budget na Economic Council-IBEC) afisini mwake mtaani Karen, Dkt Ruto aliahidi kufanya mazungumzo na uongozi wa bunge ili kukwamua mvutano huo kuhusu ugavi wa mapato.
“Huu mvutano kati ya wabunge na maseneta kuhusu kiasi cha pesa ambazo zinapasa kutengewa serikali za kaunti haupasi kuendelea kwani utaathiri shughuli za kaunti. Binafsi nitafanya mazungumzo na uongozi wa mabunge yote mawili kwa lengo la kupata suluhu la haraka kuhusu suala hili,” akasema.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, Msimamizi wa Bajeti (CoB) Agnes Odhiambo na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya. Magavana wengine waliohudhuria ni; Wycliffe Wangamati (Bungoma), Samuel Tunai (Narok), Ndiritu Muriithi (Laikipia), Amason Kingi (Kilifi), Sospeter Ojaamong (Busia), Ferdinand Waititu (Kiambu) na Mutahi Kahiga (Nyeri).
Wengine waliokuwepo ni mwenyekiti wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) Jane Karingai na manaibu gavana Joash Maangi (Kisii) na Titus Ntuchiu (Meru).
Mkutano huo uliafiki kuwa mkutano wa kujadili mvutano kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu kutopitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORB) ufanyike Jumatatu juma lijalo.
Wabunge wanashikilia kuwa serikali za kaunnti zitengewe Sh316 bilioni katika bajeti ya Sh3.02 trilioni iliyosomwa Alhamisi iliyopita na Waziri Rotich. Nao maseneta wanataka kaunti zigawiwe Sh327 bilioni wakisema hilo linatokana na ongezeko la kiwango cha mapato ya serikali kuu.
Mvutano huo ulipelekea Waziri Rotich kusoma bajati kabla ya kupitishwa kwa maswada huo ambao ungetoa nafasi kwa serikali za 47 za kaunti kuanza kuunda bajeti zao. Kwa sasa, kaunti hizo haziwezi kutayarisha bajeti zao kwa sababu haijabainika kiasi cha fedha ambazo zitapokea kutoka kwa Hazina ya Kitaifa katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.
Weki jana, kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale alisema baada ya kamati ya upatanishi kufeli kukubaliana kuhusu suala hilo, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi sasa ataamuru kuwasilishwa upya kwa mswada huo.