Habari

Ruto acheza chini ya maji

July 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MRENGO wa ‘Tangatanga’ serikalini sasa umeamua kutumia mbinu ya kuunga mkono maamuzi yote ya Rais Uhuru Kenyatta kama mkakati wao wa kisiasa.

Washirika wa Dkt Ruto wanasema kati ya maamuzi hayo ni kuunga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI) pamoja na kukukubali kuondolewa kwao katika vyeo vya Seneti na Bunge la Kitaifa.

Wanasiasa hao wanasema kumekuwa na njama ya kumsukuma Dkt Ruto kwenye ukuta ili aanze kupingana na Rais Kenyatta moja kwa moja na hivyo kutoa sababu ya kumwondoa ofisini.

“Sasa tumeamua kukubali kila kitu ambacho Rais Kenyatta atasema ili kuwanyima maadui wetu nafasi ya kutuchezea ngware,” mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alieleza Taifa Leo jana Jumanne.

“Uhuru alete hiyo ripoti ya BBI na kila kitu kingine anataka tumpitishie, na tutafanya hivyo asubuhi na mapema ndio tumalize hayo maneno tuelekee kwenye mambo mengine.”

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa, ambaye alisema wameamua kuwa watiifu kwa maamuzi yote ya Rais Kenyatta.

“Rais akielekeza kitu tutakuwa tukifuata kwa asilimia mia moja. Hii ni serikali yake na jukumu la kila uamuzi anaofanya ni lake binafsi. Sasa anasema BBI ni kitu kizuri kwa Wakenya, na sisi pia tunasema ni kizuri zaidi kwa kuwa tumeng’amua sisi ndio wa kunufaika zaidi kutokana na hiyo BBI,” akasema Bw Ichung’wa

Alisema kuwa harakati za Rais Kenyatta za kutimua wandani wa Dkt Ruto kutoka nyadhifa za Seneti na Bunge ulikuwa ni uchokozi ili kumsukuma katika makabiliano na bosi wake.

“Ruto alitushawishi tujiepushe kujibu matukio hayo. Tangu hapo tuliamua kukubaliana na lolote Uhuru na washirika wake wanasema. Hii imewanyima makombora ya kutuangamiza,” akasema mbunge huyo wa Kikuyu.

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri pia aliunga mkono kauli hiyo akisema BBI kama anavyosisitiza Rais Kenyatta ni mpango mzuri na unafaa kupitishwa na Wakenya wote.

KUKANGANYA MAADUI

“Sasa ni miaka miwili inaelekea kuisha tangu watwambie kuhusu BBI. Rais amesema iko sawa na sisi tunamwambia ailete haraka tuipitishe,” akasema Bw Ngunjiri.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, naye alisema BBI ina manufaa kwa mrengo wa Dkt Ruto kwani hata wao watapata fursa ya kubuni muungano wa kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Prof Ngugi Njoroge aliambia Taifa Leo kuwa Dkt Ruto amekuwa na busara kwa kuamua kujiepusha na makabiliano ya moja kwa moja na maadui wake wa siasa, hali ambayo inawafanya kushindwa kufahamu anachopanga na pia imewafanya raia wengi wamhurumie kwa kuwa kimya chake kimetoa picha ya “mtu anayeonewa bure”.

Prof Njoroge alieleza kuwa uamuzi wa Tangatanga kukumbatia BBI pia utafanya siasa dhidi ya Dkt Ruto kukosa makali, na zaidi ya hayo itamfaa kuunda muungano na maeneo ambayo hayajaingizwa katika muungano wa Rais Kenyatta, Odinga, Moi na Kalonzo.

KUSALITIWA

“Kuna uwezekano wa Ruto kunasa wanasiasa wakubwa wa Magharibi. Pia vigogo kama Aden Duale na wengine kutoka jamii ndogondogo ambao wanajihisi kusalitiwa na Rais Kenyatta watapata kimbilio ndani ya basi la Ruto,” akasema.

Kulingana na Prof Njoroge, Rais Kenyatta ndiye yuko na kibarua kigumu cha kushikilia muungano ambao tayari amebuni na Mabw Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moi wa Kanu, lakini kwa upande mwingine, anaeleza Dkt Ruto ana kibarua rahisi cha kuunda muungano wake bila presha.