Ruto aeleza jinsi urafiki wake na Rais Kenyatta ulivyokolea
Na SAMMY WAWERU
URAFIKI baina yangu na Rais Uhuru Kenyatta haujaanza leo wala jana ila ni wa kuanzia kitambo, hii ndiyo kauli ya Naibu wa Rais Dkt William Ruto.
Dkt Ruto Alhamisi usiku kwenye mahojiano na runinga ya NTV, alifichua kuwa urafiki wake na Rais Kenyatta ulianza chini ya utawala wa Rais (mstaafu) Daniel Arap Moi, pale kiongozi huyo alianza kumuandaa Kenyatta kujiunga na ulingo wa siasa.
“Nilijuana na Uhuru Kenyatta kupitia Rais mstaafu Daniel Arap Moi mnamo 1998,” alisema Naibu Rais.
Kwenye simulizi yake, Ruto alisema Moi alituma Mark Too ambaye kwa sasa ni marehemu na ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge maalum wa chama cha Kanu, kushawishi Ruto kuruhusu nafasi yake itwaliwe na Kenyatta.
Bw Kenyatta, aliingia kama mbunge maalum, na 2002 akawania urais kwa tiketi ya Kanu kupitia uungwaji mkono na Moi, Dkt Ruto akisisitiza kuwa alisimama kidete na Kenyatta.
Katika kinyang’anyiro hicho, Kenyatta alibwagwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki, ambaye alitawala hadi 2013.
Katika mahojiano hayo, yaliyoendeshwa na mtangazaji Ken Mijungu, Ruto alisema urafiki wake na Rais Kenyatta ulisababisha wawili hao kuungana 2013, kuwania kiti cha urais na kuahidi kuunganisha taifa, ambalo lilikuwa limegawanyika kufuatia ghasia za uchaguzi mkuu wa 2007. Zaidi ya watu 1, 300 waliuawa na maelfu kufurushwa makwao.
Hata ingawa Dkt Ruto hakueleza bayana ikiwa walikuwa na mkataba kati yake na Rais Kenyatta, Kenyatta atawale mihula miwili, halafu amuunge mkono 2022 kumrithi, Naibu Rais alisema hakuweka ‘sheria na kanuni’ zozote za urithi wa Ikulu.
“Nilipomuunga mkono Uhuru Kenyatta sikufanya hivyo ili aniunge baadaye katika azma yangu kuwania urais. Sikuweka sheria zozote zile,” alifafanua.
Chini ya mrengo tawala wa Jubilee, Ruto alisema ni chama kinachothamini demokrasia, “na atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya urais 2022, Rais Kenyatta atamuunga mkono, na si Uhuru Kenyatta pekee pia mimi nitamuunga mkono”.
Kwenye mahojiano hayo yaliyosheheni mengi, Dkt Ruto alieleza kushangazwa kwake na jina lake kila siku kuwa katika katikati ya mdahalo wa siasa. Baadhi ya viongozi, hasa wa upinzani wamekuwa wakimtaka Naibu Rais kueleza anakotoa pesa za michango kila wikendi makanisani na katika harambee.
Swali la Ken Mijungu, “Eleza umma thamani ya utajiri wako” lilionekana kumghadhabisha Dkt Ruto akishangaa “mtoto wa maskini hawezi kuwania urais nchini?”.
“Yaelekea mimi ndiye mwanasiasa anayeulizwa swali hili. Ina maana kuwa mtoto wa maskini hawezi kuwania urais?” Ruto akajibu swali kwa swali.