Habari

Ruto aendelea kupata kipigo kortini licha ya genge la washauri

Na SAM KIPLAGAT May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto jana aliendelea kupata pigo kortini huku akipoteza kesi mbili ambazo zinahusiana na miradi ya kimsingi ya utawala wake.

Jana, Mahakama ilisimamisha Kamati iliyoteuliwa na Waziri wa Afya Aden Duale kuchunguza na kutathmini deni ambalo lilisalia wakati Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) ilikuwa ikitumika kwa wanaosaka matibabu.

Pia bado kortini, mradi wa nyumba za gharama nafuu ulipata pigo eneo la Langáta, Nairobi, Mahakama ya Mazingira iliposimamimisha ujenzi wa nyumba 15,950 za gharama nafuu.

Kuhusu NHIF ambayo nafasi yake imechukuliwa na Bima ya Afya ya Kijamii (SHA), mahakama ilipiga breki jopo la kuchunguza deni hilo ikisema katiba lazima izingatiwe.

Raia wanne wakiongozwa na Dkt Magare Gikenyi, walipinga kutathminiwa au kukaguliwa kwa deni ambalo NHIF ilikuwa nayo ikisema jukumu hilo la kikatiba ni la Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Rais Ruto mnamo Machi 5 aliagiza kamati hiyo ibuniwe kuchunguza jinsi deni ambalo NHIF inadaiwa liliafikiwa.

Aliamrisha hospitali ambazo zinadai NHIF chini ya Sh10 milioni zilipwe mara moja huku zile ambazo zinadai zaidi ya kiwango hicho zisubiri utathmini wa kina.

Wakati huo, kulikuwa na malalamishi kutoka hospitali za kibinafsi kuhusu madeni waliyodai NHIF na hata wakasitisha utoaji wa huduma kwa Wakenya waliosajiliwa na SHA.

Kamati hiyo ilibuniwa mnamo Machi 28 na Bw Duale, ikiwa na wanachama 19 na ikaongozwa na James Msairo Ojee.

Kamati yenyewe ilikuwa ikague madeni ya NHIF kuanzia Julai 2022 hadi Septemba 2024. Dkt Gikenyi na waliowasilisha kesi kortini walisema hatua hiyo inakiuka jukumu la Mkaguzi wa Hesabu za serikali.

“Amri ya muda inatolewa kuzuia kamati hii isiendelee na kazi yake kwa sababu kuna ushindani kati ya umma na taasisi za kiafya ambazo zilikuwa zimetia saini makubaliano ya kutoa huduma na NHIF,” akasema Jaji Reuben Nyakundi.

Aliamrisha kesi hiyo isikizwe Juni 2. Jaji Nyakundi pia alisema waliowasilisha kesi wameibua maswali kuhusu kuwekwa wazi kwa rekodi za kimatibabu za wagonjwa kuafikia kiwango cha fedha zilizotumika.

Alisema hiyo inakiuka haki ya wagonjwa wao na ni jambo ambalo likianikwa hakuna njia yoyote ya kuzuia athari zake.

Pia Dkt Gikenyi alisema jopo la Bw Ojee lilibuniwa bila msingi wowote wa kisheria au kikatiba huku akisema wajibu huo ni Mkaguzi wa Bajeti.

Isitoshe, mtaalamu huyo wa masuala ya kimatibabu alisema hakukuwa na mkutano wa ushirikishaji wa umma kuhusu kuteuliwa kwa kamati hiyo.

Kwake Bi Gikenyi, Bw Duale hana mamlaka yoyote ya kikatiba kuajiri mfanyakazi kwa afisi ya mkaguzi wa bajeti ya serikali.

“Uteuzi wa makamishina hao tisa kutekeleza jukumu la mkaguzi wa bajeti na afisi yake ni ukiukaji mkubwa wa katiba,” akaongeza Bi Gikenyi.

Alisisitiza kwamba, ni ubadhirifu wa fedha za umma kwa kazi moja kutekelezwa na asasi mbili za umma na akashangaa kwa nini notisi ya gazeti haikuweka wazi kiwango cha malipo kwa wanachama wa kamati hiyo.