Ruto afunika ODM
USHAWISHI unaoendelea kuongezeka wa Rais William Ruto katika ngome za jadi za ODM na uhasama kati ya viongozi wake unaendelea kulemaza umaarufu wa chama hicho.
Haya yanafanyika huku ODM ikijiandaa kushiriki mazungumzo na UDA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027.
Wachanganuzi wa siasa wanasema kosa kubwa la ODM lilikuwa kuwaelekeza wafuasi wake kumuunga mkono Rais Ruto kutafuta muhula wa pili kabla ya kukubaliana kuhusu masharti ya ushirikiano wa kisiasa kati ya vyama hivyo.
Wanasema ODM ilipaswa kwanza kujadiliana na UDA na kuweka masharti ya ushirikiano katika makubaliano rasmi kabla ya kuwaomba wafuasi wake kumuunga Rais.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho pia wamekuwa wakitoa ahadi binafsi zinazodhoofisha msimamo wake rasmi katika mazungumzo. Hali hii imezua hofu kuwa ODM inaweza kukosa nafasi ya kupata maslahi yake katika serikali ijayo.
Tangu UDA ianze kushirikiana na marehemu Raila Odinga mnamo 2024, Rais Ruto na washirika wake wamekuwa wakijenga miundo ya kisiasa na kuwavutia viongozi wa mashinani katika maeneo yaliyokuwa ngome za ODM.
Miradi ya maendeleo ya serikali pia imeongeza ushawishi wa Ruto katika maeneo hayo. Baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM sasa wanamuunga mkono Rais bila masharti, huku wakipinga msimamo rasmi wa chama.
Hali hiyo imeonekana zaidi Nyanza, ambako viongozi kadhaa wa ODM wamekuwa wakifuatana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, katika hafla za umma na kutangaza kumuunga mkono Rais Ruto.
Ndani ya ODM sasa kuna mgawanyiko kuhusu iwapo chama hicho kinapaswa kutia saini makubaliano rasmi na UDA au kuendelea kumuunga Rais kwa nia njema ya kisiasa.
Nguvu za chama katika mazungumzo pia zinadhoofishwa na viongozi wake wakuu walio katika Baraza la Mawaziri la Ruto, wakiwemo John Mbadi, Opiyo Wandayi, Wycliffe Oparanya, Beatrice Askul na Hassan Joho.
Wachanganuzi wanasema mawaziri hao wana maslahi ya kisiasa katika kuhakikisha serikali ya Kenya Kwanza inaendelea kutawala baada ya 2027.
Zaidi ya hayo, baadhi ya viongozi wanapigania nafasi ya mgombea mwenza wa Rais Ruto, huku Bw Mbadi akitangaza azma ya kuwania urais mnamo 2032.
Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga amewaonya viongozi wa chama hicho dhidi ya migawanyiko inayoweza kudhoofisha msimamo wao katika mazungumzo.
“Ninawaomba viongozi wote wa ODM kuzungumza kwa sauti moja, kama watu wamoja, chini ya uongozi mmoja. Hatuwezi kujiruhusu kugawanywa na maslahi binafsi au matamshi ya kiholela yanayodhoofisha nguvu zetu za pamoja za majadiliano,” akasema Dkt Oginga akihutubia mkutano wa Jacaranda Jumamosi.
“Nguvu zetu zimekuwa katika umoja wetu, na ni lazima tulinde mshikamano huo kwa kila hali,” akaongeza.
Dkt Oginga pia alikosoa viongozi wanaojihusisha na mipango ya urithi wa kisiasa wa 2032 badala ya kuangazia uchaguzi wa 2027.
“Tuangalie vipaumbele vyetu na ninaona viongozi wengi wakipoteza muda muhimu wakijadili uchaguzi wa 2032. Huo ni usumbufu hatuwezi kumudu. Lazima tuzingatie uchaguzi wa 2027,” akasema.
Hata hivyo, Bw Mbadi aliwaambia wataalamu kutoka Kano kuwa anajiandaa kuwania urais mnamo 2032, akisema hatapoteza nguvu zake kutafuta nafasi ya Naibu Rais ambayo alidokeza haina mamlaka makubwa katika uendeshaji wa nchi.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed, ni miongoni mwa viongozi wanaosisitiza kuwa ushirikiano wa ODM na UDA lazima uandikwe rasmi.
“ODM na UDA zitakuwa na serikali ya muungano iliyoandikwa rasmi, huku vyama viwili vikishirikiana kuunda serikali ijayo. Hakuna kitu kinachoitwa nia njema pekee. Hakuna uungwaji mkono usio na masharti. Lazima makubaliano yaandikwe,” akasema Bw Mohamed.
Gavana wa Kisii Simba Arati pia alisisitiza kuwa ODM haitakubali kuingia serikalini bila masharti.
“Watu wanasema hatupaswi kumwekea masharti Rais William Ruto. Sisi kama ODM tunasema lazima kuwe na makubaliano na masharti yatakayowezesha chama kuingia serikalini,” akasema.
Lakini baadhi ya viongozi, akiwemo Mbunge wa Nyando Jared Okello, wanapinga msimamo huo. Wanasema ODM inapaswa kumuunga mkono Ruto ili eneo hilo linufaike na miradi ya serikali.
“Tunahitaji kufungua mioyo yetu na kuwa pamoja na Rais ili viongozi wengine wa upinzani watakapokuja watukute tayari tuko naye. Kwa sasa tunanufaika na miradi iliyoanzishwa na serikali hii, ilhali hatukumchagua,” akasema Bw Okello.
Alitilia shaka umuhimu wa mikataba ya kisiasa, akitaja kile alichokiita usaliti wa kisiasa uliowahi kutokea kati ya viongozi wa zamani.
Mchangunizi wa siasa na mhadhiri wa chuo kikuu Amerika, Profesa David Monda, alisema timu inayoongozwa na Bw Sifuna imechukua nafasi ya kisiasa iliyokuwa ikihusishwa na kundi la Dkt Oginga.
“Ni kama wao ndio wana roho ya Raila kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakishabikiwa,” akasema Profesa Monda.