HabariSiasa

Ruto alia wandani wake kuadhibiwa na Rais

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU Rais Dkt William Ruto mnamo Jumamosi alivunja kimya chake kuhusu masaibu yanayowaandama wabunge wanaomuunga mkono huku akimshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kulenga kumkata miguu kisiasa.

Wandani wa Dkt Ruto waliondolewa kwenye uongozi wa mabunge ya Seneti na Kitaifa huku wengine wakivuliwa uanachama kwenye kamati za bunge.

Naibu Rais alisema waliotimuliwa waliadhibiwa bila kosa lolote isipokuwa tu kwa kumuunga mkono kwenye azma yake ya kuingia Ikulu 2022

Dkt Ruto alisema hayo nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu alipokutana na Baraza la Maaskofu wa Bonde la Ufa.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na mkewe Bi Rachel Ruto, wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Caleb Kositany (Soy), Kimani Ngunjiri (Bahati) na Gladys Shollei (Mwakili wa Wanawake wa Uasin Gishu).

Dkt Ruto aliwasihi maaskofu hao wawaombee wandani wake aliosema wanahangaishwa kutokana na msimamo wao wa kisiasa.

“Katika Kenya ya sasa, watu wengi wanatishwa kwamba watapelekwa mahakamani, wengine kwa mamlaka za KRA, EACC huku wengine wakiambiwa wataondolewa afisini. Hawajatenda kosa lolote lakini wanaandamwa kwa sababu wao ni wandani wangu. Hata mimi ni Mkenya,” akasema Dkt Ruto.

Alilalamika kwamba migawanyiko ya kisiasa ambayo imeshuhudiwa nchini miaka ya nyuma imechangia taifa kutopiga hatua kimaendeleo.

“Siasa za migawanyiko na kikabila zimeanza kurejea polepole nchini. Watu wanatishwa na wengine wanashurutishwa wakubali kuunga mkono mrengo fulani kisiasa,” akaongeza Naibu Rais.

Huu ulikuwa mkutano wa pili wa maombi Dkt Ruto alikuwa akiandaa Uasin Gishu baada ya ule wa Ijumaa.

Viongozi hao wa kidini nao walimsihi Rais Kenyatta afungue nchi ili wananchi warejelee shughuli zao za kawaida lakini kwa kuzingatia maagizo ya kujizuia kuambukizwa na kusambaza virusi vya corona.