HabariSiasa

Ruto aona mwanya wa kuanza kutangatanga tena

July 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais, Dkt William Ruto Alhamisi alidokeza kuwa ataanza ziara zake sehemu mbalimbali nchini hivi karibuni kufuatia kulegezwa kwa marufuku ya usafiri kutokana na janga la corona.

Ziara nyingi za Dkt Ruto na wafuasi wake mashinani, almaarufu kama Tangatanga, zilizimwa tangu janga la corona lilipoingia nchini.

Kwa wiki kadhaa sasa, Naibu Rais amelazimika kukutana na viongozi wa kijamii, wanasiasa, viongozi wa kidini na vijana nyumbani kwake Karen, Kaunti ya Nairobi au Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alipozungumza jana akitoa misaada ya vifaa mbalimbali kwa makundi ya vijana na wanawake katika makazi yake Karen jana, Dkt Ruto alisema amefikia uamuzi wa kujiandaa kurudi mashinani kwa vile ameombwa kufanya hivyo na vijana.

“Kwa sasa mambo ya corona yamelegezwa kidogo. Nitawatembelea alivyoomba huyu mungwana hapa ili nijionee biashara na shughuli zingine mnazofanya kujipatia riziki,” akasema Dkt Ruto.Licha ya kuwa Rais Uhuru Kenyatta alilegeza baadhi ya kanuni za kuzuia uenezaji virusi vya corona, marufuku ya mikutano ya kisiasa ingali ipo.

Kila wiki, Naibu Rais hutoa misaada kama vile mitambo ya kuosha magari, mashine ya ususi, mitambo ya kushona nguo, miongoni mwa vifaa vinginevyo, kwa makundi ya vijana kutoka maeneo bunge kadhaa ya Nairobi.

Ijapokuwa yeye husema misaada hiyo ni ya kuinua vijana kiriziki, wadadisi wanaamini anaandaa ‘jeshi’ la kuvumisha sifa zake mashinani anapojiandaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.’Huu si wakati wa siasa, huo wakati utafika baadaye,’ alisema jana.

Alikuwa ameandamana na Seneta Maalum Millicent Omanga na wabunge Nixon Korir (Langata), George Theuri (Embakasi Magharibi) na James Gathiru (Embakasi Mashariki).

Wakati huo huo, mwandani wake sasa wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta aharakishe kutoa ripoti ya Mpango wa Maridhiano.Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany jana alidai kuna njama ya kisiasa inayozuia kutolewa kwa ripoti hiyo.

Alisema wanachama wa kundi la Tangatanga wako tayari kwa mapendekezo yoyote ya jopokazi hilo lililoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji.

“Tunataka watutolee ripoti ya BBI badala ya kujaribu kuitumia kucheza siasa. Tunajua wanatafuta wale ambao wataipinga; wailete tu hamna atakayeipinga,” akasema Bw Kositany ambaye amegeuka msemaji wa mrengo huo wa Dkt Ruto.

Wiki iliyopita, Seneta Haji alisema wamekamilisha kazi ya kuandaa ripoti hiyo na kwamba wataiwasilisha kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga, “wakati ambapo wawili hao watakuwa tayari.”

Imedaiwa kuwa shughuli hiyo imecheleweshwa kutokana na hali kwamba Bw Odinga yuko Dubai ambako anaendelea kupata afueni baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hii ina maana kuwa Wakenya watasubiri hadi arejee nchini kabla ya ripoti hiyo kutolewa. Wiki jana Bw Odinga aliahidi kurejea shughuli zake za kisiasa “hivi karibuni.”

Lakini Mbunge wa Keiyo Kusni Daniel jana aliambia Taifa Leo kwamba huenda Rais na Bw Odinga wameingiwa na wasiwasi kutoka na ufichuzi wao kwamba wanaunga mkono wazo la kuanzishwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi kwani utawafaa kubuni ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema wakereketwa wa BBI wamekuwa wakiendeleza propaganda kwamba Dkt Ruto anapinga juhudi za kuunganisha taifa, kupitia ripoti ya BBI.

“Kwa kuwa sasa wamegundua kuwa Naibu Rais anaunga mkono wazo hilo, sasa wanasaka kisingio kingine kabla ya kutolewa kwa ripoti hiyo,” akasema Bw Rono.

Aidha, Mbunge huyo anabashiri kuwa huenda Rais Kenyatta na Bw Odinga wametofautiana kuhusu baadhi ya mapendekezo kwenye ripoti hiyo na sasa wanaichelewesha ili kutoa nafasi ya wao kukubaliana.