Habari

Ruto aongoza Wakenya kuutazama mwili wa Raila

Na WINNIE ONYANDO October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto Oktoba 16, 2025 aliongoza Wakenya katika shughuli ya kuutazama mwili wa Waziri wa zamani Raila Odinga na kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo mashuhuri katika uwanja wa Moi Kasarani.

Rais alifuatwa na familia ya Bw Odinga ikijumuisha Mama Ida Odinga na wanawe.

Aliyekuwa rais wa zamani Uhuru Kenyatta pia alifuata kuutazama mwili wa kiongozi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Wengine waliofuata ni Edwin Sifuna, Milly Odhiambo, gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen, Babu Owino pamoja na mawaziri wengine.

Sanduku ya marehemu ilikuwa imefunikwa na bendera ya Kenya kuashirika ushujaa wake.

Mamia pia walifurika nje wakisubiri kwa hamu kuuona mwili wa Baba huku wakipiga mayowe na kupeperusha bendera na matawi.

Shughuli hiyo iliwezekana baada ya maafisa wa usalama kuwaondoa kwa nguvu waombolezaji waliojitokeza kwa wingi katika uwanja huo kumuaga Bw Odinga.

Mwili wa Bw Odinga ulisindikizwa na mamia kutoka uwanja wa ndege wa JKIA hadi Kasarani na umati mkubwa.

Tangu habari za kifo chake kutangazwa, serikali imempa heshima za kipekee Bw Odinga ikijumuisha benderea zote kupeperushwa nusu mlingoti, ndege iliyoubeba mwili wake kubadilishwa jina na kuitwa RAO001.