Ruto aonya Malala kwa ‘kulisha’ watoto siasa
RAIS William Ruto amewataka walimu na wazazi kuwakinga watoto dhidi ya watu aliowataja kama wenye nia mbaya ya “kuvuruga akili zao changa”.
Akionekana kurejelea mzozo uliogubika mchezo wa kuigiza, “Echoes of War” (Mwangwi wa Vita) katika Tamasha ya Kitaifa ya Michezo ya Kuigiza baina ya Shule na Vyuo jijini Nakuru wiki jana, Dkt Ruto alionya dhidi ya majaribio ya watu fulani kuwafundisha wanafunzi itikadi potovu na siasa mbaya.
“Sharti tuwakinge watoto wetu kutokana na wanaolenga kuwanyanyasa kingono, walanguzi wa dawa za kulevya na wale wanaotaka kuvuruga bongo zao kwa kuwafundisha kuwachukia wazazi wao, walimu, viongozi na taifa lao. Sharti tuwalinde watoto wetu dhidi ya waovu hawa wote,” Rais Ruto akaeleza jana kwenye Ibada ya makanisa mbalimbali katika kijiji Kipng’etik, kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Dkt Ruto alisema hayo siku chache baada ya wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere Echoes of War katika tamasha hizo kwa kusheheni maudhui yanayoakisi maovu ya serikali ya sasa.
Mchezo huo wa kuigiza ulioandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala, hasa unaangazia juhudi za vijana wa Gen Z kupigania utawala bora.
Bw Malala, ambaye pia ni seneta wa zamani wa Kakamega alikamatwa Jumatano usiku.
Aliachiliwa baada ya kuzuiliwa usiku kucha katika Kituo cha Polisi cha Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo huku tukio hilo likiibua kero kubwa miongoni mwa mashirika ya kutetea haki na wanasiasa.
Wanafunzi wa Butere walilalamikia kukamatwa kwa Bw Malala, mwelekezi wao, na wakasusia kuigiza mchezo huo chini ya masharti yaliyowekwa na serikali.
Maafisa wa polisi walishutumiwa kwa kuwarushia vitoza machozi wanafunzi hao na kuwashambulia wanahabari walifika katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kirobon, Nakuru, eneo la tukio.
Baada ya kuachiliwa, Bw Malala alielekeza kidole cha lawama kwa Rais Ruto akidai ndiye aliamuru kuzimwa kwa mchezo huo wa kuigiza.
“Ikiwa washauri wako hawawezi kukuambia, wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere walitaka kukuambia kuwa wanataka utawala bora, wanachukuia ufisadi na ukiukaji wa haki za kibinadamu,” Bw Malala alisema.
Hata hivyo, mawaziri Kipchumba Murkomen (Usalama) na Julius Migos Ogamba, walimtetea Rais Ruto wakisisitiza kuwa serikali haitaruhusu watoto kutumiwa kuendeleza vita vya kisiasa.
“Serikali haijatishwa na mchezo wa kuigiza, Echoes of War na haina nia ya kuuzima. Kile tunapinga ni kuhusishwa kwa wanasiasa katika masomo ya watoto wetu na wao kupewa nafasi ya kuingiza ajenda zao za kisiasa hata katika sanaa,” Bw Murkomen akasema Alhamisi akiwa katika ziara ya usalama Kaunti ya Tana River.
Jana, Rais Ruto alisisitiza kuwa watoto wanafaa kupewa nafasi ya kunawiri katika nyanja za elimu, michezo na sanaa bila kuvurugwa kwa kufunzwa itikadi mbovu.
“Sharti tuwape watoto wetu nafasi ya kunawiri katika fani mbalimbali. Wajiendeleze katika masomo ya kawaida, yale ya kiufundi, sanaa, michezo na nyanja nyingine zinazohitaji vipaji na ujuzi. Serikali yangu imejitolea kuhakikisha kuwa tunaafikia lengo hili,” akasema.
Kiongozi wa taifa, kwa mara nyingine, aliwataka wazazi kuwafundisha watoto wao maadili mema na wawaonyesha dhidi ya kutumia mitandao ya kijamii kueneza chuki na matusi.
“Watoto wetu watumia mitandao kujizalishia mapato,” Dkt Ruto akasema.
Mnamo Jumamosi, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Kiongozi wa chama cha Roots Party George Wajackoyah walimshauri Rais Ruto kuwazuia watu fulani wanaoipa serikali yake sifa mbaya kwa kuendeleza vitendo vya ukiukaji haki.
“Baadhi ya maafisa wako wanafanya kazi yake kuwa ngumu bila sababu yoyote. Kwa mfano, mbona walileta drama nyingi Nakuru na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere?” Bw Sifuna akauliza.
Kwa upande wake, Profesa Wajackoyah alimshauri Rais Ruto kuwaita wanafunzi na mwalimu wao mkuu ili kuridhiana nao.
“Mheshimiwa rais ili wanafunzi hawa wasiendelee kukuchukia kwa kosa ambalo huenda silo lako, waite Ikulu pamoja na Mwalimu wao Mkuu na upatane tena na wao,” akasema katika Shule ya Upili ya Ramba wakati wa Ibada ya mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa Raila Odinga, George Oduor.