Ruto arejea nyumbani kuzima moto
WYCLIFF KIPSANG na BARNABAS BII
KUONGEZEKA kwa umaarufu wa kisiasa wa Seneta Gideon Moi wa Baringo eneo la Rift Valley kumemlazimu Naibu Rais William Ruto kurudi katika ngome yake ya kisiasa kupambana na hali hiyo.
Bw Moi amekuwa akiendeleza siasa mashinani kupitia kwa wanasiasa, wazee na mabwenyenye wa Rift Valley, hali ambayo imempa ushawishi mkubwa siku za karibuni katika jamii ya Kalenjin.
Duru zilisema Bw Moi na washirika wake walichukua fursa ya Dkt Ruto kutokuwepo nyumbani kufuta umaaruru wake Rift Valley.
Baada ya kugundua mambo yamemharibikia nyumbani, Dkt Ruto ameanza msururu wa ziara Rift Valley na tayari amezuru kaunti za Nandi na Uasin Gishu mara mbili ndani ya wiki moja katika juhudi za kubadilisha mkondo wa upepo.
Dkt Ruto ametumia muda mwingi kuzuru maeneo ya Mlima Kenya, Pwani, Magharibi na sehemu za Nyanza akiongoza kundi la Tanga Tanga kujipigia debe kwa ajili ya 2022 na hajakuwa akionekana sana Rift Valley.
Uasi dhidi yake umeongezeka baada ya baadhi ya wanasiasa na mabwenyenye waliokuwa wakimuunga mkono kuonekana kuhamia kambi ya Bw Moi ambaye ni mwenyekiti wa Kanu.
Hatua ya Chama cha Mashinani (CCM) cha aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto kuegemea upande wa Bw Moi pia imekuwa pigo kwa Naibu Rais.
Cha kumtia wasiwasi zaidi ni kuwa Bw Moi amekuwa akikutana na wanasiasa pamoja na viongozi wenye ushawishi kutoka eneo la Sugoi, ambako ni nyumbani kwa Naibu Rais.
Wiki iliyopita, Bw Moi alikutana na viongozi kadhaa wa Bonde la Ufa katika eneo la Kabarak katika juhudi za kujitafutia uungwaji mkono kabla ya kinyang’anyiro cha urais cha 2022.
Miongoni mwa waliokutana na Bw Moi ni Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, ambaye amekuwa akirushiana cheche za maneno na Seneta wa kaunti hiyo Kipchumba Murkomen ambaye ni mwandani mkuu wa Naibu wa Rais.
Japo Bw Tolgos anasisitiza kuwa angali ndani ya chama cha Jubilee na anaheshimu Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto, amekuwa akimmiminia sifa tele Seneta Moi.
“Napenda namna Gideon Moi anaendesha mambo yake. Anapenda kila mtu na wala hatumii matusi; ana tabia sawa na mimi,” Gavana Tolgos aliambia Taifa Leo.
Wengine waliohudhuria kikao cha Kabarak ni wabunge Sila Tiren (Moiben), Wilson Sossion (Kuteuliwa) na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat.
Wengine ni wabunge wa zamani Zakayo Cheruiyot, Musa Sirma, Frankline Bett, Bw Isaac Ruto, mwanasiasa Zedekiah Bundotich maarufu Buzeki na mbunge wa Tiaty William Kamket.
Kushuka kwa umaarufu wa Naibu Rais katika ngome yake ndilo pigo la majuzi kabisa kumkabili kwenye safari yake ya kujiimarisha kwa ajili ya kuwania urais 2022.
Tayari kundi la wanasiasa wanaomuunga mkono la Tanga Tanga limeonekana kutuliza siasa baada ya kukabiliwa vikali na maafisa wa serikali akiwemo Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe.
Umaarufu wake pia umefifia Pwani ambako mwaka jana alifanya kampeni kali za kushawishi wabunge wa ODM kumuunga mkono, lakini sasa wametulia.