Ruto aruka mtego wa Joho
Na VALENTINE OBARA na FARHIYA HUSSEIN
UJANJA wa Gavana Hassan Joho wa Mombasa kujaribu kumshurutisha Naibu Rais William Ruto atangaze kuunga mkono handisheki na shughuli za Jopo la Maridhiano (BBI), uligonga mwamba Jumapili wakati wa sherehe za Mashujaa katika Kaunti ya Mombasa.
Wakati wa sherehe hizo zilizoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, viongozi waliozungumza waligusia umuhimu wa handisheki ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga isipokuwa Dkt Ruto.
Katika hotuba yake, Bw Joho alionekana kukashifu wapinzani wa handisheki, ambao wengi wao ni wanasiasa wa Jubilee wanaoegemea upande wa Dkt Ruto.
Alipochukua nafasi ya kumwalika Dkt Ruto jukwaani kuhutubia umma, gavana huyo alisema: “Namwalika Naibu Rais aunge mkono handisheki,” akasema huku akimsalimia kwa mkono.
Dkt Ruto hupinga shughuli za BBI kwa misingi kuwa mchakato huo unatumiwa na Bw Odinga kuleta mabadiliko ya katiba ambayo yatasababisha kuwepo nafasi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa pamoja na manaibu wake.
Ingawa yeye husema hatua hiyo itasababisha hasara kwa wananchi kugharamia mishahara na marupurupu ya viongozi zaidi, wadadisi wa kisiasa husema hofu yake ni kwamba mamlaka ya rais yatapunguzwa endapo hilo litapitishwa ilhali anatazamia kumrithi Rais Kenyatta ifikapo 2022.
Naibu Rais aliepuka kabisa kuzungumzia mambo ya handisheki bali akasisitiza kwamba kile kinachoweza kuleta mabadiliko yanayotamaniwa nchini ni utekelezaji kikamilifu wa Ajenda Nne Kuu za maendeleo zilizoanzishwa na serikali.
“Lazima tukabiliane na umasikini na ukosefu wa ajira. Ajenda Nne Kuu za maendeleo pekee ndizo zitatatua changamoto zinawazokumba Wakenya hasa vijana. Ninaamini tunafuata njia bora zaidi kupitia kwa ajenda hizo. Tusikubali uchochezi na utapeli wa kisiasa,” akasema huku akitoa wito viongozi wamuunge mkono Rais kwa juhudi zake.
Rais Kenyatta alisubiriwa na wengi kuhutubia umma kando na hotuba yake iliyoandaliwa mapema, lakini hakufanya hivyo na kuwaacha wananchi hoi.
Kwa kawaida, Rais hutoa hotuba ya Kiswahili kwa umma baada ya kusoma hotuba yake rasmi ya Kiingereza lakini hali ikawa tofauti Jumapili.
Kwenye hotuba yake alipigia debe muafaka wake na Bw Odinga akisema hata utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu unategemea mafanikio ya BBI.
Kulingana naye, handisheki ilionyesha bado kuna viongozi nchini wanaojitolea mhanga kutetea masilahi ya wananchi bila kujali faida zao za kibinafsi sawa na ilivyokuwa kwa waliopigania uhuru kutoka kwa Wakoloni.
“Kenya imefika katika awamu muhimu mno ya ustawi wake. Maamuzi ambayo yatafanywa hivi sasa ndiyo yataamua kama tutatimiza maono yetu ya Ruwaza ya 2030 au hata Ajenda Nne Kuu za maendeleo,” akasema.