HabariHabari za Kitaifa

Ruto arukia viongozi wa upinzani, asema demokrasia na uhuru viandamane na maendeleo

Na MARY WANGARI October 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto alitumia hotuba yake ya kuadhimisha Mashujaa Dei kusuta vinara wa upinzani wakiongozwa na vuguvugu la Linda Mwananchi ambapo aliwakejeli kwa kutafuta mamlaka bila mpango halisi.

Katika ujumbe wake uliorejelea wapinzani wake hasa kinara wa The Equitable Party, Seneta Edwin Sifuna, Rais Ruto alisisitiza kwamba ushindani unapaswa kujikita kwenye sera na mipango thabiti badala ya migawanyiko, ukabila na kushambulia mahasimu.

Akizungumza jana katika sherehe zilizofanyika Kipchoge Keino, Eldoret, Rais alionya kuhusu tishio la viongozi wanaojishughulisha kusaka mamlaka bila mpango thabiti akisema huenda wakakosa kuwajibika baadaye. “Kila kiongozi anapaswa kuwa tayari kuwasilisha rekodi na maono thabiti kuhusu wanapotaka kupeleka nchi ikiwemo mpango madhubuti kuhusu jinsi ya kufika hapo,” alisema Rais Ruto. Huku akinukuu kifungu cha Biblia, Rais alihoji kwamba demokrasia na uhuru hauna maana iwapo hautaboresha nafasi za kujiendeleza kiuchumi, kuboresha huduma za umma na maisha ya wanajamii kwa jumla.

“Jinsi maandiko yanavyotukumbusha, imani bila matendo imekufa. Vivyo hivyo, uhuru na demokrasia bila maendeleo na ufanisi ni bure,” alisema Rais.

“Wajibu wetu si kuhifadhi tu uhuru tuliorithi, bali kuhakikisha unageuka kuwa hadhi, nafasi na maisha bora kwa Wakenya.”

Aidha, alitumia hotuba yake kupigia mageuzi kiuchumi yaliyofanikishwa na serikali yake kupitia miradi mikuu kama vile mpango wa nyumba za bei nafuu, afya, kilimo, ujenzi na ukarabati wa miundomsingi.

Alitaja ukosefu wa kazi, barabara duni na ukosefu wa huduma za afya miongoni mwa vizingiti vikuu kwa Wakenya akiwakashifu wapinzani wake kwa kupinga miradi ya Kenya Kwanza bila kutoa suluhisho mbadala.

“Unapendekeza nini kando na unachopinga? Alihoji.

“Kama unatofautiana na nyumba za bei nafuu, eleza Wakenya jinsi utakavyowapa makazi bora na kuunda nafasi za kazi.”

“Ikiwa unapinga mageuzi yetu ya huduma za afya, fafanua utakavyohakikisha kwmaba hakuna familia itakayolazimishwa kuchangisha pesa ili kulipa bili ya hospitali.:

 

‎