Habari

Ruto asema nia ya wabaya wake ni kumpaka tope

March 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

NAIBU Rais William Ruto amesema Jumamosi kwamba mauaji ya Sajini Kipyegon Kenei ni njama za mahasimu wake kumpiga vita na kulemaza azma yake kisiasa huku akiwaeleza washindani wake kwamba hawatafanikiwa kamwe ila tu kwa kumuua.

Akitoa salamu za pole katika hafla ya mazishi ya marehemu iliyofanyika Nakuru, Bw Ruto amesema kwamba anafahamu vyema kwamba kuna njama za kumzuia kwa kila hali kuhusu Uchaguzi Mkuu 2022 akisema yuko imara na hatikisiki.

“Wale wanaoendesha njama hizi nataka niwaeleze ya kwamba pengine waniue mimi lakini sitarudi nyuma. Siwezi kurudi nyuma kwa sababu Kenya ni ya Wakenya wote. Kenya si ya Wakenya wachache. Vitisho, njama hizi zote na hata yale mambo yanayokuja hapo mbele ambayo yamepangwa ninayafahamu lakini niko tayari,” amesema Ruto.

Bw Ruto amesema juhudi za washindani wake kisiasa za kuzua uhasama baina yake na wanajamii kutoka ngome yake ya kisiasa eneo la Bonde la Ufa kwa kumuua afisa wake kutoka Solai zitaambulia patupu.

“Kama mliua huyu ndiyo mnitishe mimi nataka niwaambie damu ya huyu itawaandama hamtapona. Ninajua ninachokisema; mimi ni Naibu Rais wa Kenya, mimi si mwendawazimu. Wale wanaopanga hivi tu njama eti watanipiganisha mimi na jamii yangu, shauri yao,” akasema.

Aidha, Dkt Ruto amemshutumu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) dhidi ya kutumiwa na mahasimu wake kisiasa kudunisha Afisi ya Naibu Rais na badala yake akamtaka azingatie kazi yake ya kuchunguza masuala ya uhalifu.

“Mimi nataka kumwambia Bw DCI tafadhali fanya kazi ya askari. Chunguza, tafuta ukweli; siasa achana naye kwa sababu hii njama inaundwa ya kisiasa. DCI anatumiwa kwa sababu za kisiasa kudunisha afisi yangu, kunivuta chini na baadhi hata hawana aibu kusema kwamba William Ruto hatakuwepo 2022 na ilhali wako huru,” amesema.

Amesema pia anamtegemea Mungu zaidi.

“Ninafahamu na ninajua kwamba kuna njama kuu ambayo imepangwa kudhalilisha na kuharibu afisi yangu na kuhakikisha kwamba sitafika popote, Hilo ninajua na ni wazi. Wanaokula njama hiyo ili kunizuia kwa kutumia mbinu zote hizi, nataka kuwaambia, wanaweza kuwa na mfumo na vyote hivyo lakini tuna Mungu,” amesema katika chapisho katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Amewataka wanaomwandama kisiasa kupambana naye binafsi badala ya kuwahusisha watu wengine huku akisema kwamba marehemu Kenei alifariki kutokana na vita vya kisiasa dhidi yake.

“Wakati tuna huzuni nyingi ya kuuawa kwa huyu kijana, kuna watu wengi wanipiga vita vya kisiasa. Nataka niwaambie wanaonipiga vita vya kisiasa, wanipige mimi waachane na watu wengine. Mwanamume huyu aliyelala hapa alikuwa afisa wangu. Kifo ambacho huyu jamaa amekufa ni kwa sababu ya mambo haya yanayozungushwa,” akasema.

Aidha, Naibu Rais ametoa maelezo kuhusu nyakati za mwisho za marehemu Kenei pamoja na mazungumzo ya mwisho baina yao kabla ya mwili wake kupatikana eneo la Imara Daima, Nairobi akiwa ameuawa kinyama.

Amesema kwamba alizungumza na marehemu, siku tatu tu kabla ya kupatikana akiwa ameuawa.

Kulingana na Bw Ruto, alikutana na Bw Kenei pamoja na maafisa wengine wawili waliokuwa wakifanya kazi katika majengo ya Naibu Rais akitaka kuarifiwa kuhusu yaliyokuwa yamejiri wakati wa mkutano wa aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa.