RAIS William Ruto alisherehekea Sikukuu ya Krismasi akiwa kwenye makazi yake ya kifahari mjini, Kilgoris, Kaunti ya Narok, pamoja na Mama Taifa, Rachel Ruto.

Bw Ruto alitua Kilgoris mnamo Jumatano baada ya kuhudhuria karamu ya Krismasi katika mbuga ya Maasai Mara.

Alhamisi asubuhi, Desemba 25, 2025, Rais pamoja na mke wake walihudhuria ibada ya Krismasi katika kanisa la PEFA Ikarian Cathedral lililopo Lolgorian, Kilgoris.

Kupitia ujumbe wa pamoja, Rais na Mama Taifa walihimiza kuwepo kwa umoja, amani na uwiano katika msimu huu wa sherehe.

“Kuzaliwa kwa Yesu Kristu kulete matumaini, furaha na amani makazini mwenu. Tunaposherehekea, tukumbatiane pamoja na baraka zinazotuunganisha kama taifa moja,” alisema Kiongozi wa Taifa.

Katika ibada hiyo kanisani, Rais Ruto aliandamana na naibu waziri wa zamani Magerer Lang’at na viongozi wengine wa eneo hilo.

Baada ya ibada, familia ya rais ilitangamana na waumini, kabla ya kiongozi huyo wa nchi kuondoka.

Duru zilieleza Taifa Leo kuwa Rais Ruto baadaye alitumia siku hiyo kukagua shamba lake kubwa.

Katika siku za majuzi, Ruto amechagua makazi yake ya kifahari ya Kilgoris, kuwa sehemu anayopendelea zaidi ambapo amesherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na familia yake kwa miaka mitatu iliyopita na vilevile kuwakaribisha wageni rasmi katika hafla kadhaa.

Kiongozi wa Taifa anafahamika kuwa na makazi manne ya kibinafsi yaliyopo kaunti za Nairobi, Uasin Gishu na Taita Taveta.

Hata hivyo, makazi yake ya Narok yamkini ndiyo fahari yake mpya, yakiangaziwa kitaifa katika siku za karibuni.

Rais Ruto, ambaye ni mwanafunzi wa siasa wa rais wa pili nchini Kenya, Daniel arap Moi, yamkini amegeukia kupenda makazi yake ya Kilgoris, sawa tu na hayati rais Moi alivyoenzi makazi yake ya Kabarak, katika kaunti ya Nakuru.

Anageuza taratibu makazi yake Kilgoris kuwa ngome ya mamlaka.

Kwa miaka 24 ambayo rais wa zamani Moi alitamalaki siasa za Kenya, makazi yake ya kifahari yaliyojengwa kwenye ekari 2,300, mjini Kabarak, Nakuru yalisalia ngome yake ya mamlaka na kituo kikuu cha siasa za taifa.

Katika utawala wake, Kabarak iligeuka kuwa kituo salama, ambapo angejiliwaza kutoka vigogo wa mamlaka jijini Nairobi. Hamna shaka Moi alipenda Nakuru.

Alipotaka kuepuka purukushani za jiji kuu Nairobi, angeelekea Kabarak.

Ilikuwa karibu ni hakika kwamba Mzee Moi angezuru Nakuru siku za wikendi na sherehe za Mwaka Mpya.