Ruto atupia ODM mistari kuhusu 2027
RAIS William Ruto amesema kuwa hesabu zake za kisiasa za 2027 zitashirikisha ODM huku akisisitiza kuwa chama hicho lazima kidumishe falsafa ya uongozi wa marehemu kinara wake Raila Odinga.
Kiongozi wa nchi alisema kuwa malipo pekee ambayo anaweza kumlipa Bw Odinga ni kuhakikisha kuwa ODM inasalia serikalini na ifikapo 2027, chama hicho kinabuni serikali au kuwa kwenye muungano ambao utatawala.
“Tulipobuni ODM tulitaka kubadilisha mfumo wa siasa za nchi hii ndiyo maana hiki chama kina utambulisho na malengo wala hakijikiti kwenye siasa za ukabila,” akasema Rais Ruto.
“Nilikuwa na mazungumzo na Raila na kitu kimoja ambacho aliniambia ni kuwa katika siasa ushindani si uadui. Jiulizeni kwa nini Raila alifanya kazi na (Daniel) Moi, (Mwai) Kibaki, Uhuru (Kenyatta) na William Ruto,” akasema Rais Ruto.
Rais alikuwa akiongea jijini Mombasa Novemba 14 usiku kama mgeni wa heshima katika dhifa ya kuadhimisha miaka 20 ya ODM. Hafla hiyo iliandaliwa kumuenzi Bw Odinga aliyeaga dunia Oktoba 15 akiwa nchini India.
Alisema kuwa ODM imehimili mawimbi makali ya kisiasa tangu 2005 na chama hicho hakifai kusambaratika kwa sababu Raila hayuko.
“Mimi nina mizizi yangu ODM na hata kama hupendi, huo ndio ukweli. Huwezi kuandika stori yangu bila kutaja ODM. Mnasema nirudi nyumbani na niko nyumbani tayari?” akauliza Rais huku waliohudhuria dhifa hiyo wakimtaka ajiunge tena na chama hicho na kumshangilia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, wafuasi na waanzilishi wa chama ambao walisimulia safari yao tangu 2005.
“Sijuti kuwa sasa ODM na UDA zinaendesha Serikali Jumuishi. Si tusukume haya maneno tuende mbele?” akauliza.
Kiongozi wa nchi alifichua kuwa pamoja na Prof Hino na Prof Anyang’ Nyong’o kwa ushauri wa Odinga, waliandaa mkutano kuhusu jinsi ambavyo Kenya inaweza kupiga hatua hadi kuwa katika tapo la mataifa yaliyopiga hatua kiuchumi.
“Lazima niwaambie familia ya ODM, lazima tufanye kazi pamoja kusongesha nchi hii mbele jinsi tulivyokubaliana na Raila. Nina imani kuwa kwa kuungana, tutainua nchi hii hadi kiwango kingine kiuchumi.”
“Kwa Dkt Oginga, una nafasi ya kuongoza chama hiki vizuri na kutoshea viatu vya Raila. Najua hukuwa ndugu yake bali pia mtu wake wa siri kwa sababu katika kila suala alikuwa akitegemea ushauri wako,” akasema Rais.
Alifichua kuwa Dkt Oginga ndiye alikuwa mhimili muhimu katika kubuniwa kwa Serikali Jumuishi na akawataka wanachama wa ODM wamuunge mkono.
“Hamtakosa nafasi ya kufikia serikali hata bila uwepo wa Raila. Nafurahia sana mchango wa wanachama wa ODM kwenye utawala huu na kila kitu kinafanywa kwa kuzingatia manifesto ya hiki chama,” akasema huku akimrejelea Waziri wa Fedha John Mbadi.
Dkt Oginga aliwaongoza viongozi wanaogemea mrengo wa serikali ndani ya ODM kusema wataendelea kushirikiana na serikali hadi 2027.
“Hakuna chama hapa duniani kinachobuniwa kuwa kwenye upinzani, vyama vyote huwa vinapigana kuwa serikalini. ODM haijaachwa nyuma na sasa tuko serikalini na mbeleni kama ODM au muungano lazima tuwe serikalini,” akasema Dkt Oginga.
“Hata sisi tunataka mamlaka huwezi kusema tu tuko. Tutatekeleza sera zetu vipi kama hatutaki mamlaka na tunaenda maandamano?” akauliza Dkt Oginga.
Hayo yalijiri huku baadhi ya viongozi wa chama hicho wakipinga ushirikiano wa ODM na UDA.
Mnamo Ijumaa, bintiye Raila Winnie Odinga na Gavana James Orengo walionekana kupinga ushirikiano wa chama cha serikali wakisema ODM itaendelea na mapambano ya kupigania raia wa chini.