Ruto: Hata mkisema ‘wantam’ sina shida, najua kazi yangu itanipa ‘two-term’
RAIS William Ruto Jumapili aliwakemea wakosoaji wake akisema mradi tu atimize ahadi zake za maendeleo kwa Wakenya, ana hakika ya kuchaguliwa tena mnamo 2027.
Kiongozi wa nchi alisema kuwa serikali yake kwa sasa inatekeleza miradi kadhaa ya kuimarisha miundomsingi, kubadilisha sura ya jiji na kuimarisha maisha ya wakazi wa Nairobi pamoja na kwingineko nchini.
Rais alisema zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wamekuwa wakiishi kwa vitongoji duni na utawala wake unamakinika kuhakikisha kuwa mradi wa nyumba za gharama nafuu unafaulu hasa kwenye vitongoji hivyo.
“Ni matumaini yangu kwamba kupitia mradi huu, hatutabadilisha Nairobi pekee bali pia maeneo mengine ya taifa letu,”’ akasema.
Alikuwa akiongea baada ya kuhudhuria ibada ya kanisa Kibera ambapo alisema serikali inalenga kujenga zaidi ya nyumba 60,000 Nairobi pekee.
Wiki iliyopita, Rais aliwapa wakazi wa Mukuru nyumba ambazo ujenzi wao ulikuwa umekamilishwa.
“Tuwapuuze wapinzani wetu ambao hawana chochote cha kuwapa Wakenya ila tu wamebobea kwenye matusi, ukabila na kusaka umbeya. Tumakinikie kujenga nchi yetu,” akaongeza.
“Mimi haja yangu ni kuhakikisha Wakenya wameungana tena uongozi wangu ubadilishe maisha yao. Hilo ndilo jambo la lazima kwangu,” akasema.
Alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa akiwemo Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye alitumia nafasi hiyo kutoa wito wa mageuzi kuhusu jinsi serikali inavyoshughulikia majanga ya dharura hasa visa vya moto.
“Wiki hii tumepoteza maisha ya watu 15 kutokana na mikasa ya moto. Kulikuwa na mikasa hiyo Mathare, Makina hapa Kibera kisha mtoto pia aliteketea motoni mtaa wa Reuben. Lazima tufanye jambo na kuweka mikakati ya kuvumbua mbinu ya kupambana na mikasa hii,” akasema Bw Sakaja.