Ruto hatakikani Jubilee – Wabunge
ONYANGO K’ONYANGO Na BENSON MATHEKA
WABUNGE wanaomuunga Naibu Rais William Ruto katika vuguguvu la Tangatanga, sasa wanadai kuwa hatakiwi katika chama cha Jubilee ili kutoa nafasi kwa Rais Uhuru Kenyatta kuendelea kuhudumu.
Kulingana na wabunge hao, kuna mipango ya kumzuia Dkt Ruto kutumia chama hicho kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Matamshi yao yanajiri chini ya miezi miwili kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wa maafisa wake kuanzia mashinani hadi kitaifa na tetesi kuwa Rais Kenyatta anataka mageuzi ya kikatiba ili ashikilie wadhifa wa Waziri Mkuu.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi na mwenzake wa Keiyo Kusini Daniel Rono, wabunge hao walisema matamshi ya aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa chama hicho David Murathe na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Francis Atwoli kwamba Rais Kenyatta atakuwa Waziri Mkuu, yalinuiwa kuhujumu azima ya kugombea urais ya Dkt Ruto.
Mnamo Jumatano mbunge wa Kandara Alice Wahome ambaye ni mwanachama wa ‘Tangatanga’ pia alisema matamshi ya Bw Murathe na Bw Atwoli yana ukweli.
“Nashindwa kuelewa kwa nini Rais amekubali kupotoshwa na watu kama Murathe na Atwoli badala ya kurekebisha uchumi ambao unakaribia kuzama na kuzua msukosuko wa kijamii, watu hawa wanatumiwa kumhujumu Dkt Ruto na ndio sababu kila wakati wanasema kuwa hakupatia chama cha Jubilee kura kilichoshinda uchaguzi mara mbili,” Bw Sudi aliambia wanahabari Jumamosi mjini Eldoret.
Bw Murathe na Atwoli walisema kwamba huenda Rais Kenyatta akabakia mamlakani katika wadhifa tofauti baada ya kupindi chake cha pili kama rais kumalizika 2022.
“Kile ambacho Rais hawezi kufanya ni kugombea urais lakini chini ya mageuzi mapya ya kisiasa kupitia Jopokazi la Maridhiano (BBI), tunatarajia kuwepo kwa miungano mipya ya kisiasa itakayohusisha wote,” Bw Murathe alisema kwenye mahojiano na ‘Taifa Jumapili’.
Jumamosi, Bw Sudi alimtaka Rais kujitokeza na kutangaza wazi iwapo anataka kubaki mamlakani badala ya kutumia vibaraka wa kisiasa.
“Rais ninayemfahamu huenda asiwe na nia ya kubakia mamlakani inavyodaiwa na Murathe, lakini iwapo anataka, wacha ajisemee mwenyewe na tunaweza kuwa na mazungumzo kuhusu hilo,”alisema mbunge huyo.
Naye Bw Rono alisema kwamba wanachukulia matamshi ya Bw Murathe kwa uzito sana na kudai kuwa Rais anayaunga mkono.
“Hatuwezi kupuuza Murathe aliyosema majuzi, ni mwandani wa karibu wa Rais Kenyatta na anatumiwa kupima hali. Tunajua kwamba anataka kukwamilia mamlakani kupitia wadhifa unaobatizwa Waziri Mkuu na huenda akabadilisha nia akitambua kuwa hatua hiyo inapingwa na wengi,” Bw Rono aliambia ‘Taifa Jumapili’ kwa simu.
Bw Rono alisema Rais na mshirika wake katika handisheki, kiongozi wa ODM Raila Odinga wanadanganya nchi kwamba BBI ni ya kuunganisha Wakenya ilhali ni yao kujitafutia nyadhifa.
Wandani wa Dkt Ruto wanasema kuna njama za kuwazuia kushiriki uchaguzi wa Jubilee mwezi Machi ili asipate tiketi ya chama hicho ya kugombea urais.
Ingawa Katibu Mkuu wa chama Raphael Tuju anasisitiza kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki, mbunge wa Nyeri mjini ambaye ni mwanachama wa kundi la Kieleweke linalompiga Dkt Ruto anasema ni wanachama waliodhihirisha nia ya kusaidia Rais Kenyatta kutimiza ajenda zake na kuacha kumbukumbu watakaoshiriki uchaguzi huo.
Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakipinga maamuzi ya Rais na serikali na ‘Kieleweke’ wanawalaumu kwa kuhujumu Rais Kenyatta.
“Ninatarajia kuwa ni watu watakaochukua nyadhifa za kusimamia chama ni wale ambao wamedhihirisha kwa asilimia 100 kwamba wanaunga na kutekeleza sera za Rais Kenyatta kama kupigana na ufisadi na kuunganisha Wakenya,” alisema Bw Ngunjiri.