Ruto, Kalonzo, Oburu wawatakia Wakenya Krismasi njema
RAIS William Ruto, Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ni kati ya viongozi wakuu ambao wamewatakia Wakenya Krismasi njema huku wakiwataka wote kuhakikisha usalama barabarani na umoja wa nchi.
Kwenye video iliyosambaa mitandaoni, Rais Ruto akionekana mwenye furaha, aliwashukuru Wakenya akisema kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu wanaelekea kukamilisha mwaka huu.
“Wakenya 2025, tunaumaliza na nawatakia Krismasi njema na Mwaka Mpya wa 2026 wenye baraka. Kule barabarani tuendeshe kwa makini na tujiepushe kuvunja sheria.”
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka aliyekuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa Desemba 24, alitumia siku hiyo kurai wananchi.
“Tuwakumbuke wasiojiweza na familia zinazoendelea kuwaomboleza wanao waliokufa kwenye ajali ya barabarani. Pia tuwakumbuke Gen Z waliopoteza maisha yao na wahanga wa ghasia za kijamii eneo la Trans Mara.”
Dkt Oginga ambaye atasherehekea Krismasi nyumbani kwake Bondo, alitoa wito kwa Wakenya waungane na kumakinikia ujenzi wa taifa lao.
Hii itakuwa Krismasi ya kwanza bila Kiongozi wa ODM na kigogo wa siasa za upinzani Raila Odinga.
Kwenye Krismasi za nyuma, Dkt Oginga na Bw Odinga wamekuwa wakihudhuria ibada ya Krismasi kwenye Kanisa la Kianglikana (ACK) Nyamira, Bondo.