Habari

Ruto kusuka upya serikali baada ya kifo cha Raila

Na DAVID MWERE October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto anatarajiwa kufanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri wakati wowote, ili kumpa nafasi Mwenyekiti wa chama cha KANU, Gideon Moi, ambaye amekuwa mwanachama mpya katika  serikali jumuishi.

Watu wa karibu na Rais wameeleza Taifa Leo kwamba mabadiliko hayo yameharakishwa  kufuatia kifo cha kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ambaye mwaka jana alikuwa mhimili muhimu katika juhudi za Rais Ruto kutuliza maandamano ya kizazi cha Gen Z yaliyotishia utawala wake.

Kifo cha Bw Odinga kimeacha pengo kubwa la kisiasa na kuvuruga usawa wa nguvu uliokuwa umebuniwa chini ya serikali jumuishi. Sasa, Rais Ruto anakabiliwa na jukumu la kupanga upya serikali yake kudumisha uthabiti wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Katibu Mkuu wa KANU, George Wainaina, amethibitisha ushirikiano unaoendelea kati ya viongozi hao wawili, akielezea mpango huo kama “ushirikiano wa umoja, usio wa ulafi wa madaraka.”

“Wataalamu wetu wa chama wanaendelea kukamilisha maelezo ya makubaliano hayo mapya, ambayo yatafanya washirika kadhaa wa Moi kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali serikalini. Hata hivyo, makubaliano haya hayahusu manufaa ya kisiasa, bali umoja wa kitaifa,” alisema Bw Wainaina.

Makubaliano hayo, ambayo yanatarajiwa kutiwa saini na Rais Ruto na Bw Moi hivi karibuni, yatarejesha chama cha KANU katikati ya uongozi wa serikali baada ya miaka mingi katika baridi ya kisiasa. Hatua hiyo inadaiwa kuwa shukrani kwa uamuzi wa Moi kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha useneta  Baringo katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27.

Wachambuzi wanasema kuingia kwa Moi serikalini kunaimarisha juhudi za Rais Ruto za kujenga serikali jumuishi na kufufua uhusiano na familia ya Moi — uhusiano ambao kwa miongo kadhaa umejawa na ushindani na maridhiano ya mara kwa mara.

Habari zinaonyesha kuwa makubaliano hayo yalisukwa baada ya mikutano mitatu muhimu kati ya viongozi hao wawili — miwili nchini Kenya na mmoja Dubai mwezi uliopita.

Hata hivyo, Bw Wainaina alisema: “KANU haitafuti vyeo. Tunataka kuona maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.”

Vyanzo vya karibu na mazungumzo hayo vimefichua kwamba Moi anaweza kuteuliwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi, wadhifa unaoshikiliwa kwa sasa na Davis Chirchir, ambaye ni rafiki wa karibu wa Rais Ruto.

Chanzo kingine kilifichua kuwa marehemu Raila Odinga ndiye aliyeratibu hatua za awali za kuwaunganisha Rais Ruto na Moi, ingawa hakubahatika kushuhudia matunda yake.

Makubaliano hayo yanadaiwa pia kujumuisha uteuzi wa wafuasi wa Moi katika nyadhifa za makatibu wakuu, mabalozi, na wakurugenzi wa mashirika ya umma.

Miongoni mwa wanaotajwa ni Gladwell Tungo, aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Baringo; Ibrahim Sheikh, Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti wa KANU kutoka Kaskazini Mashariki; na Samuel Poghisio, aliyewahi kuwa Waziri. Pia wametajwa Ali Khan, msaidizi wa muda mrefu wa Moi, na Eddie Kivuvani, Mweka Hazina wa chama hicho.

Licha ya madai hayo, Bw Wainaina alisema: “Iwapo nafasi zitatokea na wanachama wetu watafaidika, hilo ni jambo jema, lakini si sababu ya sisi kujiunga na serikali  jumuishi.”

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Bw Moi anaweza pia kuteuliwa Naibu  Mkuu wa Mawaziri, nafasi ambayo itamfanya kuwa kiongozi wa nne wa ngazi ya juu serikalini baada ya Rais Ruto, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi..

Vyanzo vingine vimedokeza kuwa sehemu ya makubaliano hayo inahusisha kulipwa kwa madeni ya takriban Sh3 bilioni  ambayo kampuni za Moi inadai serikali katika sekta ya Kawi.

Kwa mujibu wa mshirika wake wa karibu, “Moi alihisi kuchoshwa na kucheleweshwa kwa malipo yake na kudaiwa ushuru kwa fedha ambazo hakuwa amepokea.”

Wachambuzi wa siasa wanasema “mkono wa maridhiano” kati ya Rais Ruto na Moi ni sehemu ya mkakati mpana wa Rais kuunda serikali jumuishi, inayolenga kuleta viongozi kutoka pande zote za kisiasa ili kuimarisha umoja wa taifa na kujiweka vizuri kwa uchaguzi wa 2027.

Rais Ruto, katika hotuba yake huko Kabarak mwezi Septemba, alisisitiza kuwa juhudi hizo hazihusu siasa za kugawana mamlaka bali ni harakati za kuharakisha maendeleo

“Hili si suala la watu binafsi au maeneo. Ni kuhusu Kenya. Nimeanzisha serikali jumuishi kwa sababu nchi inahitaji mikono zaidi ya kuleta maendeleo.”