Sababu 11 Ruto hatajiuzulu
Na BENSON MATHEKA
WALIVALIA shati na tai zinazofanana ungedhani ni sare za Ikulu.
Wakakagua miradi ya maendeleo pamoja na hata wakati mmoja naibu rais akachukua usukani kama kaimu rais. Yote hayo ni kabla ya uhasama wa sasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto.
Na sasa, Dkt Ruto amesukumwa pembeni na baadhi wamemtaja kama mtazamaji katika serikali aliyopigana kufa kupona kuiunda. Swali ambalo limo vinywani mwa Wakenya wengi ni, kwa nini hajiuzulu na kuanzisha rasmi mchakato wa kutwaa mamlaka kutoka kwa bosi wake baadaye 2022?
Wadadisi na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa tuliozungumza nao waliafikiana kwa kauli moja kwamba, Dkt Ruto hatajiuzulu hadi muda wake wa kuhudumu ukamilike. Kwanza, anahofia kujiuzulu licha ya kutengwa serikalini kwa kuwa anahofia kupoteza hadhi na minofu anayopata akiwa mamlakani.
Isitoshe, wadhifa huo unampa ushawishi mkubwa kote nchini anaotumia kujenga himaya yake ya kisiasa. Kujiuzulu kutamaanisha atapoteza afisi yake ya kifahari iliyoko mtaani Karen ambako amekuwa akitumia kuandaa hafla na kutembelewa na jumbe za viongozi wa kisiasa na wa kidini kutoka kote nchini na makundi ya kisiasa.
Wadhifa wake, unamhakikishia usalama wa hali ya juu, familia yake na mali yake ambayo imetapakaa kote nchini.
Afisi hiyo pamoja na boma zake za kibinafsi jijini Nairobi na Sugoi kaunti ya Uasin Gishu zinalindwa na maafisa wa GSU waliopatiwa mafunzo ya kulinda watu mashuhuri. Akiwa Naibu Rais, Dkt Ruto na familia yake hulindwa na kikosi cha Recce ambacho vile vile humlinda rais.
Shamba lake kubwa katika kaunti ya Taita Taveta pia linalindwa na maafisa wa usalama. Kote anakoenda, anasindikizwa na walinzi wanaoondoa msafara wake wa magari ya kifahari kuepuka msongamano, fursa ambayo atapoteza akijiuzulu.
Kwa miaka saba ambayo amekuwa Naibu Rais, Dkt Ruto na familia yake wanafurahia bima ya matibabu kutoka kwa serikali. Yote hayo yatayeyuka siku hiyo hiyo ataamua kujiuzulu.
Bajeti ya afisi ya Dkt Ruto mwaka huu ni Sh1.8 bilioni ambazo atazikosa kwa miaka miwili akijiuzulu. Ametengewa Sh34 milioni za safari za nje ya nchi, Sh98 milioni za ziara za humu nchini na Sh103 milioni za petroli ya magari yake na Sh 25 milioni kuburudisha wageni wanaomtembelea.
Mkewe pia ametengewa Sh52 milioni, zikiwemo Sh17 milioni za burudani katika bajeti ya mwaka huu ambazo atakosa iwapo mumewe atajiuzulu.
Heshima ya afisi hiyo ya pili kwa hadhi nchini inamfanya kudumisha mitandao ya washirika wa kisiasa na kibiashara ambao anaweza kuwapoteza wakati huu anaazimia kugombea urais 2022. Anatumia afisi hiyo kulinda na kupanua himaya yake ya biashara ndani na nje ya nchi. Washirika wake wa kisiasa wanamkwamilia kwa sababu ya wadhifa wake na anafahamu kwamba, wanaweza kumtelekeza akijiuzulu.
Dkt Ruto amehusishwa na madai ya ufisadi, ukiwemo unyakuzi wa mashamba kama ardhi ilikojengwa hoteli ya Weston jijini Nairobi na kujiuzulu kwake wakati huu kutamweka katika hatari ya kushtakiwa kwa sababu atakuwa amejivua mamlaka yanayompatia kinga.
Dkt Ruto anatumia magari na hata ndege za serikali anapotembelea maeneo tofauti ambayo atapoteza akijiuzulu. Anapotembelea nchi za kigeni, anapokelewa kwa heshima na taadhima na kupewa ulinzi wa hali ya juu kama mmoja wa viongozi wakuu wa nchi ambao atapoteza akijiuzulu.
“Akijiuzulu ushawishi wake utapungua. Kwa wakati huu, anatumia ushawishi wa wadhifa wake wa naibu rais kuvutia uungwaji mkono ambao atapoteza mara moja,” asema mdadisi wa siasa Martin Andati.
Kwa wakati huu, Dkt Ruto ndiye kiongozi wa ngazi ya juu na msemaji wa jamii ya Wakalenjin atakuwa amewavunja moyo kwa kujiuzulu.
Shinikizo za kumtaka Dkt Ruto kujiuzulu zimeongezeka kutoka kwa viongozi wanaounga handisheki ya Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.
Viongozi hao wamefufua miito ya kumsukuma ang’atuke afisini wakisema, hawezi kukosoa serikali anayohudumia.
Wito huu umeshika kazi baada ya Dkt Ruto kukosoa serikali kwa kutumia polisi kutimiza ajenda za kisiasa na kutowachukulia hatua waliohusika katika sakata ya wizi wa corona.
Dkt Ruto pia ametengwa katika serikali, haalikwi katika mikutano ya Baraza la mawaziri na baraza la taifa la usalama. Amevuliwa majukumu yote ya wadhifa wake kama msaidizi rasmi wa Rais na alichobakishiwa ni jina la wadhifa huo kwa kuwa katiba inamlinda na hawezi kufutwa kazi na rais.
Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema, licha ya kudharauliwa, kutengwa na kugeuka mkosoaji wa serikali, itakuwa vigumu kwa Dkt Ruto kujiuzulu miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.
Kulingana na Sebastian Opande, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa na utawala, Dkt Ruto akijiuzulu wakati huu, atakuwa ameonyesha kushindwa mapema.
“Ruto ana uzoefu wa siasa wa miaka mingi na anaelewa kwamba akijiuzulu miaka miwili kabla ya uchaguzi, atakuwa amekubaliana na mahasimu wake kwa kila jambo na kitakachofuata ni kuandamwa ili akatwe kucha kabisa kabla ya 2022,” asema.
Aidha, anasema akijiuzulu atawapoteza viongozi ambao wamekuwa wakimuidhinisha kugombea urais 2022.
“Anatumia wadhifa na afisi ya Naibu Rais kujenga mtandao wa marafiki na washirika mashinani lakini akisalimu amri, atawapoteza wote na itakuwa pigo kwa azima yake ya kugombea urais,” aeleza.
Wandani wake wanasema anaamini alisaidia kujenga serikali ya Jubilee na atafurahia matunda yake hadi mwisho.
“Hatuna nia ya kuondoka katika serikali ya Jubilee ambayo tulipigania kwa hali na nguvu zetu,” Mbunge wa Soy, Caleb Kositany ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto amekuwa akisisitiza.
Mara kwa mara, Dkt Ruto amenukuliwa akisema kuwa, anajua njama anazopangiwa na wanaompiga vita kwa lengo la kuzima azima yake ya kuwa Rais.
“Najua wanayopanga kule mbele, lakini mimi sitarudi nyuma, labda waniue mimi,” alisema alipohudhuria mazishi ya Kipyegon Kenei, aliyekuwa mkuu wa walinzi katika afisi yake.
Wiki jana, alisema haogopi njama zinazodaiwa kupangwa na watu walio na ushawishi serikalini kumzuia asishiriki au kushinda uchaguzi wa urais wa 2022.
Wadadisi wanasema akjiuzulu kwa wakati huu, atampisha kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi kuwa msemaji wa jamii ya Wakalenjin. Dkt Ruto anaungwa mkono na viongozi na wakazi wa ngome yake ya Rift Valley na wadadisi wanasema hii inampa nguvu za kukwamilia afisini licha ya kudhalilishwa na wadogo wake serikalini.